Ukurasa wa mbele
Gazeti la INJILI
Soma barua Yahoo
Soma barua Hotmail


Gazeti la Injili
Kwenye Internet

http://munishi.com

Tel. 254722602445 E-mail:
munishi@munishi.com


Huwezi kupewa uongozi ukiwa mgonjwa halafu ukipona uwatimue waliokusaidia. Mbaya zaidi ujiunge na chama ambacho kiliwachosha Wakenya. Ndiyo maana tulisema miaka mitano iliyopita kwamba,
KIBAKI AJICHIMBIA KABURI KISIASA
Kosa la Simba kumwachia fisi windo lake
WAKENYA WASEMA NO KWA KATIBA KIELELEZO- PIGO KWA KIBAKI

Wahenga zamani walisema, Simba ni mwindaji hodari.Akifanya kosa la kumwachia fisi windo lake, Basi mafisi wataitana kwa kicheko, na kabla simba ajue nini kinaendelea, wingi wa fisi utamzuia kujaribu kudai windo lake. Pengine arudi msituni akawinde, au afe njaa. Kusema ajaribu kunyakua windo mdomoni mwa fisi, atahatarisha maisha yake. Isitoshe mabaki aliyoacha fisi, hayafai kuliwa na yeyote.Mfupa uliomshinda FISI hata simba hauwezi. Bora akawinde. Inaonekana Raila ameamua kuwinda na tayari amepata. Kama kawaida KUNGURU Fisi na Mbwa mwitu wanajiandaa kujaribu bahati yao ili wapewe ngaa mnofu kidogo.Swali ambalo wengi wanajiuliza ni je safari hii atakubali kuachia windo lake kwa yeyote? Tunasubiri tuone.Habari zaidi

Nani angewahi kufikiri kwamba Kibaki siku moja angewahi kuwaamuru Polisi wamrushie mabomu ya machozi Raila Odinga? Mtu aliyesema KIBAKI TOSHA na akatosha. Kweli katika siasa chochote chweza kutokea. Na hatujui ni mengine gani yatakayotokea tunapoelekea uchaguzi mkuu Kenya. Ulikuwa mkutano wa Maombi ambao wahusika walikuwa na nia ya kuiombea Kenya iondokane na kivuli cha ukabila kinachotishia kuifunika Kenya. Serikali ilitumia Polisi kuupiga marufuku mkutano huo dakika za mwisho, jambo lililopelekea wahusika kuikaidi amri ya polisi na kuzusha rabsha zilizowaacha wengi wakiwa wamejeruhiwa. Je kwa nini serikali isingeruhusu mkutano huo na watoe ulinzi badala ya kuusambaratisha? Serikali inadai Usalama Nairobi umezorota na hawataruhusu mikutano yeyote jijini. Wengi wanaiona hatua ya serikali kama mbinu ya kuwakata makali ODM wanaotaka kutumia ghasia za kikabila Mathare na kwingineko kuipigisha magoti serikali. UKweli ni kwamba chuki za kikabila Kenya zimefikia kiwango cha kutisha. Tunaunga mkono hatua zozote zitakazochukuliwa na yeyote kuzuia Kenya isiufuate mkondo wa RWANDA. Na kama mkutano wa maombi ungesaidia kupooza chuki hizo, tunaishangaa serikali kuuzima kwa nguvu kupita kiasi.



KIBAKI AJICHIMBIA KABURI KISIASA
Kosa la Simba kumwachia fisi windo lake
WAKENYA WASEMA NO KWA KATIBA KIELELEZO- PIGO KWA KIBAKI


Bwana Raila mara tu baada ya tume ya uchaguzi Kenya kutangaza ushindi kwa mrengo wa chungwa Pamoja naye ni mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya Bwana Kivuitu.Wengi wametafsiri hiyo kama kura ya kutokuwa na imani na Serikali ya Kibaki.Wengine wanasema Kenya kuna marais wawili. Mmoja Rais wa matajiri wachache, yaani Kibaki, na mwingine Rais wa wananchi wote..

Raila Odinga
Wahenga zamani walisema, Simba ni mwindaji hodari.Akifanya kosa la kumwachia fisi windo lake, Basi mafisi wataitana kwa kicheko, na kabla simba ajue nini kinaendelea, wingi wa fisi utamzuia kujaribu kudai windo lake. Pengine arudi msituni akawinde, au afe njaa. Kusema ajaribu kunyakua windo mdomoni mwa fisi, atahatarisha maisha yake. Isitoshe mabaki aliyoacha fisi, hayafai kuliwa na yeyote.Mfupa uliomshinda FISI hata simba hauwezi. Bora akawinde. Inaonekana Raila ameamua kuwinda na tayari amepata. Kama kawaida KUNGURU Fisi na Mbwa mwitu wanajiandaa kujaribu bahati yao ili wapewe ngaa mnofu kidogo.Swali ambalo wengi wanajiuliza ni je safari hii atakubali kuachia windo lake kwa yeyote? Tunasubiri tuone. Kwamba mtu aliyesaidiwa kuingia ikulu atawaita WAPUMBAVU waliomsaidia, inaonyesha jinsi gani madaraka yanavyoweza kumlewesha mwanadamu akasahau alikotoka. Pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kuunga mkono udhalimu huu, bila kusahau kiburi na makidai ya serikali yaliyopelekea maisha ya baadhi ya Wakenya kupotea katika harakati za kuipinga KATIBA kielelezo ambayo ilikuwa imwongezee rais madaraka kinyume na makubaliano ya awali kwamba katiba mpya ilipaswa kuyapunguza mamlaka ya rais, bado Wakenya walionyesha kukomaa kwao kifikra, na kuikataa KATIBA hiyo mbovu. Katika hilo Wakenya wanastahili pongezi. Suala sasa siyo kutafuta wataalamu wa kuiandika katiba, bali ni kuirejelea katiba ya BOMAS na kuifanyia marekebisho kidogo halafu ipitishwe kama katiba mpya. Tatizo halikuwa utaalamu, bali ni mbinu ya wachache kuingiza vipengele vya kulinda maslahi yao kisiasa. Kwamba Wakenya waligundua janja yao, hilo ni pigo kubwa kwa kibaki na serikali yake. Hatua zozote kibaki atakazochukua zitafuatiliwa kwa makini sana na Wakenya waliokwisha umwa na NYOKA na sasa wakiguswa hata na unyasi wanashituka. Itawabidi wanasiasa wa Kenya na Afrika kwa ujumla, kubadili mbinu zao kwani upeo wa wananchi kuelewa mbambo ni wa kiwango cha juu kuliko wanasiasa walivyofikiria. Mungu Ibariki Kenya.


Wanachungwa wakisheherekea ushindi. Kibarua kigumu kiko kwa Raila. Je amwamini nani?
Ingeshangaza kama baada ya mawaziri kuupinga mradi wa serikali, wangerudi kuchukua nafasi zao Serikalini. Hatutashangazwa kama Kibaki akichukua hatua ya kuvunja baraza lake la mawaziri. Lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuwatupa waliokuwa karibu naye ili awalete wapinzani wake karibu kuwakata makali yao. Binafsi sitoshangaa kusikia Makamu wa sasa wa Rais ametupwa na badala yake wadhifa huo apewe Raila ili, kumsogesa karibu kupima nguvu zake. Kitendawili kitakuwa hapo kama Raila atakubali kupunguza umaarufu wake kwa cheo cha miaka miwili. Kulingana na matokeo ni Dhahiri Kibaki hawezi kuchaguliwa tena 2007. Kwa yeyote atakayekubali kuuza umaarufu wake kwa kazi ya miaka miwili, ataonekana kama aliyerukwa na akili. Lakini wanasiasa ni wanasiasa na chochote chaweza kutokea. Pamoja na ushindi wao kuna wale wanaosema sasa ni wakati wa kupanga mikakati mipya ya kupambana na Wakikuyu ambao wamepania kuiongoza Kenya bila kushirikiana na makabila mengine. Kwamba makabila yote 41 yataachana kwa kiwango kidogo cha kura na kabila moja hiyo inatisha. Waliokuwa wakipinga kielelezo cha katiba walipata kura 3,548,477 asilimia 57% wakati upande wa serikali ambao uliungwa mkono na Mkoa wa kati ambao ni wa Wakikuyu walipata kura 2,532,918 asilimia 43% Hii inaonyesha kwamba Wakikuyu wakiendelea na kasi walio nayo ya kuzaana, halafu watilie maanani kujiandikisha na kupiga kura kama wanavyotilia maanani biashara zao, basi makabila mengine Kenya yataongozwa na Wakikuyu wapende wasipende. Itakumbukwa kwamba Wakikuyu waliukataa mpango wa uzazi wa Serikali ya Moi wakidai kwamba ilikuwa mbinu ya kupunguza idadi yao. Siasa ni kuhusu idadi. Hatuna hakika kama hiyo ndiyo inayowapelekea Wakikuyu kuzaa kwa wingi au la. Watoto wa mitaani maarufu kwa jina la Machokoraa, wengi wao ni wa kabila hilo. Upigaji kura Afrika ni zoezi wanaloachiwa masikini. Foleni ndefu huwashinda matajiri wengi kusimama kungojea zamu yao kupiga kura. Kasumba hiyo ikibadilika, na kila dalili zinaonyesha kwamba tunaelekea hapo, basi uchaguzi na kuchaguana utategemea mambo mengi kuliko ilivyo hivi sasa.

Ilikuwa "Moi Must go", na sasa ni "Now Kibaki Must GO"

Raila amwambia Kibaki avunje bunge, kila mtu arudi mashinani kutafuta kura. Kibaki naye anaogopa kubwagwa chini, hasa kufuatia kushindwa kwake kwenye kura ya maoni.Tayari Kibaki amelivunja baraza la mawaziri kugeuza mtizamo umwelekee yeye, Lakini bado anajikuna kichwa. Inaonekana Kibaki hakuyatarajia na tayari serikali yake isiyo na mawaziri imeanza kumtupia lawama aliyekuwa rais wa Kenya Bwana Moi. Wanadai kwamba yeye ndiye anaewapa kiburi wana mrengo wa chungwa. Moi naye kwa upande wake anakana shutuma hizo. Anadai kwamba mradi wake Uhuru Kenyatta ulikataliwa vikali na Kina Raila Odinga ikapelekea chama cha KANU kushindwa vibaya 2002. Kwamba Mradi wa Kibaki yaani KATIBA KIELELEZO umekataliwa vikali na kina Raila pamoja na UHURU KENYATTA, isiwe kisingizio cha kumtupia Moi lawama. Inaonekana kama Moi anamwambia Kibaki kila mtu abebe msalaba wake. Moi kwa sasa anaishi Kabarak nyumbani kwake, inaonekana Kibaki naye atarudi Othaya hivi karibuni. Wengi wanajiuliza mbona iwe mapema hivyo kwa kibaki kurudi nyumbani? Si wangemwacha mzee Kibaki naye atuletee Uhuru wake?


"Mzee Mwenzangu Nisaidie. Maji yako shingoni"

Rais Kibaki akiwa na Rais mstaafu Daniel Arap Moi katika ikulu ya Nairobi hivi karibuni.Inasemekana Kibaki alimwita Moi kumtaka ushauri baada ya mambo kwenda mrama. Serikali ilishindwa vibaya kwenye kura ya maoni, jambo lililopelekea siasa za Kenya kubadili mkondo haraka kiasi cha Kibaki kuonekana kuhamaki na kukosa mwelekeo.Alivunja baraza la mawaziri ambalo hajui ataunda jipya la jinsi gani.Wahenga walisema "PALIPO WAZEE HAPAARIBIKI NENO. Kibaki alimuanza Mzee mwenzake kwa swali.
KIBAKI: Huyu Raila anataka kunirudisha nyumbani mapema. Nimevunja baraza la mawaziri ili nilitumie kama chambo ya kuwanasa warudi kwangu lakini naona hata hawasogelei chambo. Nifanyeje?
MOI: Waite uzungumze nao mwenyewe. Mimi siwezi kuwa mshenga kati yenu. Tena sidhani kama watanisikiliza. Mlipomkataa UHURU mradi wangu, mlikubaliana jinsi mtakavyogawana madaraka. Nasikia mlikuwa na kitu kinachoitwa MoU, Ilikuwaje? Mbona uliwazidi kete wenzako? Waite uwaombe msamaha halafu mkubaliane tena kisha muendelee. Lakini 2007 nakungoja kwenye jamvi la wazee tunywe kahawa pamoja. Pole mzee mwenzangu. Hawa vijana siku hizi wanapeleka mambo haraka sana kuliko sisi enzi zetu .
KIBAKI:
Sasa nichague nani niache nani kwenye baraza langu la mawaziri?
MOI: Hapo ni kipepeo mkononi mwako na unaniuliza kama kiko hai au kimekufa. Nikisema kiko hai utakifinya kife, useme nimeshindwa. Pia nikisema kimekufa utakiachia kiruke useme nimeshindwa. Sasa kibarua unacho mwenyewe. Kazi kwako. Ukiamua kusuka shauri yako .Ukiamua kunyoa hiari yako.Ulijua wakiikataa katiba kielelezo unayo katiba uliyoapa kuilinda na kuitetea. Itumie lakini kwa tahadhari kwani wananchi walio wengi wanaonekana wamekushtukia. Na wengi wakiamua, hakuna risasi wala jeshi litakalowazuia. Huo ndio ukweli wa mambo.

Ushikwapo Shikamana
Mawaziri 19 walikataa kutumika kwenye serikali inayoonekana kama ya KITAPELI ya Rais Kibaki.
Sababu walizotoa ni kwamba sasa hawamuamini Kibaki aliyeingia madarakani na kuanza kuvunja maagano kati ya vyama vya kisiasa vilivyoungana kuitoa KANU madarakani.Wanasema mbinu ya Kibaki imekuwa kuvimaliza nguvu vyama hivyo ili vimezwe na DP chama cha Kibaki. Kwamba waliingia kama muungano wa vyama vya upinzani kuitoa KANU, Kibaki aliwataka wakome kuwa wapinzani na watawale kulingana na masharti yake na siyo MoU waliyokubaliana mbele ya mawakili na vyombo vya habari. Tangu hapo uongozi wa Kibaki uliingia dosari ambayo sisi tuliita kujichimbia KABURI la kisiasa. Mambo yalivyo sasa ni kwamba tayari Kibaki ameanza kuingia kaburini humo na udongo unaanza kurudishwa shimoni. Akitoka, itabidi awe amemeza kiburi na kukubali kunyenyekea jambo ambalo hatumuoni msomi wa Makerere akilifanya.


Kibaki alikataa kushauriana na muungano wa vyama vilivyomuingiza madarakani na akaamua kuunda baraza jipya la mawaziri. Ajabu ni kwamba baraza hilo liliwatupa nje kina Raila na Kalonzo washika dau katika muungano wa vyama vilivyopaswa kutawala. Jambo hilo halikuwafurahisha Wakenya na ikapelekea wale walioteuliwa kuzikataa nyadhifa zao.Mawaziri 19 walikataa kutumika kwenye serikali inayoonekana kama ya KITAPELI ya Rais Kibaki.Vyama vingine vilitangaza kujiondoa kwenye muungano huo na kumfanya Kibaki abaki peke yake na chama chake cha DP. Swali ambalo wengi wanajiuliza ni kama Kibaki atamaliza muongo wake baada ya kuwageuka wenzake? Je nani aliyekuwa amemshikilia nani? muda utatuonyesha nani aliyeshikwa akakataa kushikamana.


Maua ni maua tu. Humaanisha vitu tofauti kwa watu tofauti.

Jumba la mikutano ya kimataifa KICC mahali ambapo tume ya uchaguzi ilipatumia kupokea matokeo ya uchaguzi.

Umati mkubwa wa wakereketwa wa CHUNGWA pamoja na washika dau wengine wakisikiliza matokeo kutoka tume ya uchaguzi Kenya.

Bango la tume ya uchaguzi likiwataka wakenya wapige kura kwa umakini.
Inaonekana Wakenya waliitikia mwito wa tume ya uchaguzi, kwani walisema 'NO' kwa katiba kielelezo.


Wananchi wakitoka KICC baada ya kutangaziwa matokeo ya kura ya Maoni. Wakati wa Kampeni hizo, serikali ilitumia vyombo vya habari kuwahamasisha wananchi waikubali KATIBA kielelezo bila mafanikio. Redio CITIZEN pamoja TV yake, waliipigia debe wazi wazi katiba hiyo lakini wananchi waliipiga teke. Redio na TV za CITIZEN humilikiwa na Bwana Macharia. Ilikuwa msitari wa mbele katika kuutoa utawala wa Moi, na sasa ikawa msitari wa mbele kuulinda utawala wa Kibaki. Wengine waliokuwa msitari wa mbele kuipigia debe katiba hiyo ni kampuni ya NMG wakitumia NTV pamoja na Nation FM lakini hata hivyo waligonga ukuta. Hata wao walikuwa msitari wa mbele kuung'oa utawala wa Moi, na safari hii walionekana wakiwa msitari wa mbele kumsimika kibaki mwenye madaraka mengi, ambayo hawakutaka Moi awe nayo. Hii inaonyesha kwamba wale wanaofikiri vyombo vya habari vinaweza kuwaadaa wananchi wakubali wanajidanganya wenyewe.Sasa watu wanaamua kulingana na walivyoelewa na siyo kama wanavyoambiwa na wanahabari waliopewa rushwa na wanasiasa.

Wakati wa uchaguzi Kenya kila kabila hutumia chombo chake cha habari kuhabarishana yatakayojiri. Kuna vyombo vingine vinavyojaribu kuchukua mwelekeo wa kitaifa, navyo vinajipata vikiegemea zaidi upande wa Serikali. Kawaida Serikali zote duniani siyo kipenzi cha wananchi.Vyombo vya habari vinavyoegemea zaidi upande wa serikali hujikuta vikichukiwa na wananchi walio wengi.Ukitaka kujua chombo gani kinacholinda maslahi ya wananchi ni wakati wa uchaguzi. Wakati huo ndipo utakapojua wamiliki wa vyombo vya habari.Kabla ya uchaguzi utasikia "hii ni TV yako" Lakini kampeni zikianza ndipo utakapojua kumbe TV hiyo ni ya kabila fulani. Wakati umefika kwa wanahabari kuachana na kasumba hii potovu ya kuwatumikia wanasiasa pekee na kuusahau umma.



ILIKUWA HIVI
Walikubaliana, Wakaungana, wakaitoa KANU madarakani. Inavyoonekana ni kama Kibaki amekiuka makubaliano ya MoU Picha hii ilichapishwa katika gazeti la NATION baada ya vyama vya upinzani kuungana na kuafikiana jinsi ya kuitoa KANU madarakani. Walifanikiwa, Lakini MoU mpaka leo inaleta utata.


Waliitoa KANU kwa kishindo. Waliungwa mkono na kila Mtu. Hata wanyama porini waliwaunga mkono. Miti misituni iliwaunga mkono. Ni serikali ambayo isingekuwa rahisi kumpata mpizani wake. KANU ilipata pigo ambalo isingekuwa rahisi kuamka na kuipinga serikali ya KIBAKI.

Lakini kulewa madaraka, Ukabila na kusahau fadhila, zimeifanya serikali ya Kibaki ijipasue yenyewe na ijipinge yenyewe na kujichimbia kaburi yenyewe. Inatia huruma lakini ndivyo mambo yalivyo ndani ya serikali ya Kibaki. MoU iliyowaleta madarakani Kibaki ameigeuka. Katiba waliyoahidi kuimaliza baada ya siku 100, sasa ni mwaka na nusu na hakuna dalili kwamba Kibaki anataka Katiba mpya.

Odinga aliyesema Kibaki anatosha, sasa ndiye anaeonekana kama msaliti wakati anapojaribu kuwakumbusha kibaki na wapambe wake kuhusu MoU.

Kweli dunia ina mengi. Kabla Yesu hajarudi tutaona Mengi.

Kenya iko karibu kuushuhudia uongo mkubwa ukipita mbele ya macho yao. Yaani kuyageuka maagano ya MoU. Katiba mpya waliyoahidiwa wakose kuiona, Badala ya kazi walizoahidiwa waone nyumba zao zikibomolewa, Badala ya unafuu kimaisha waone wanazidi kuwa masikini, Badala ya kuwa Taifa lifanyalo kazi, liwe ni taifa linalotembea kwa miguu baada ya sekta ya usafiri kutatizwa na sera ambazo utekelezaji wake siyo wa muda mfupi kama serikali ilivyotarajia.

Tena isitoshe waone kila siku wakati wa NEWS umeme unakatika ili wasisikie na kuona jinsi serikali ya KIBAKI inavyojichimbia kaburi, Vyombo vya habari Kenya vifikiri vinafikisha ujumbe kumbe serikali inashirikiana na kampuni ya umeme kuzima umeme wakati wa NEWS ili wananchi wasisikie yanayoendelea. Yote hayo yatakapofanyika, Ndipo msemo kwamba wanasiasa ni waongo utakapomaanisha kwa wengi.Kwangu mimi inanitatiza sana kuona watu wazima wakidanganyana mchana jua linawaka. Mungu ibariki Kenya.

Hivi ndivyo Kibaki alivyoingia madarakani baada ya kujaribu na DP mara mbili akishindwa.

Akiwa hoi bin taaban huyu ni Kibaki 2002 alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Alikuwa na majeraha mabaya aliyoyapata wakati wa kampeni huko Machakos. Wenzake walisema "KIBAKI TOSHA" Bila kujali kwamba Kapteni wao alikuwa ameumia vibaya. Yaliyofuatia yaliwashangaza wengi. Mwanzoni alijifungia Ikulu na wengi walimuelewa kwani alihitaji muda wa kuyaganga majeraha. Baada ya kile kilichojulikana kwamba sasa Kibaki ni mzima kabisa, ndipo umma ulipoanza kulisikia neno PUMBAVU kutoka kwa Rais wao. Neno hilo lilielekezwa kwa wale walioonekana kama wapinzani. Matokeo yake Kibaki amejipata katika mwanzo wa mwisho wake katika mwaka wa tatu wa utawala wake. Kama historia ya kushindwa uchaguzi mara mbili akiwa DP ndiyo iliyochangia kushindwa kwa mrengo wa ndizi, basi Kibaki peke yake hawezi kushinda uchaguzi ujao. Anawahitaji wanasiasa kutoka makabila mengine na siyo mkoa wa Kati pekee. Kama watamwamini tena tunasubiri tuone.

Wakati kuukaribia uchaguzi mkuu Niliandika makala hii

Watu kila mahali walikuwa wakiimba UPINDE na siyo upinzani ambao KIBAKI ni kiongozi wake siku nyingi. Matumaini ya upinzani kuwakomboa wakenya, yalikuwa yamefifia hasa ukitilia maanani kwamba upinzani uliwahi kushindwa mara mbili. Upinzani ndani ya KANU uliokuwa ukiongozwa na Raila pamoja na SAITOTI bila kumsahau J.J. KAMOTHO ambaye anazijua siri zote za KANU, ulionekana kama mkombozi wa kweli wa wakenya. Tuombe iwe kwamba bado unaonekana hivyo baada ya viongozi hao kukubali kuongozwa na KIBAKI aliyewahi kushindwa mara mbili. Kwangu naona hiyo imewapunguza makali viongozi wa upinde. Wa kulaumiwa ni wao wenyewe. Muda uliobaki ni mchache kulingana na yale yaliyo mbele yao kuyafanya. Nasema hayo baada ya kuyatafakari haya. KANU imetawala tangu UHURU. Usiniulize kama imekuwa ikitawala kihalali au kwa njia zisizo halali.Lakini KANU hiyo ndiyo inayowataka wakenya wamkubali UHURU kwani yenyewe ndiyo iliyoleta UHURU Kenya. Hizo njia ambazo siyo halali ndizo zinazonifanya niseme kwamba viongozi wa upinde walikosea kukubali kuongozwa na KIBAKI. Wote walitoka KANU, KIBAKI alitangulia kutoka na kuipinga bila mafanikio mara mbili. Kalonzo Musyoka na Saitoti ndio kwanza wanaanza kuipinga KANU wakiwa nje. Je ni busara kumpa kazi ya kuipinga KANU mtu aliyejaribu mara mbili akashindwa? AU wangewajaribu hawa wanaoanza kuipinga? Wanasema KIBAKI ana uzoevu wa kupinga. Sawa. Lakini pia anao uzoevu wa kushindwa.

Sahau ukabila ambao wanasiasa hutumia kwa mahesabu ya kisiasa. Pia sahau kuhusu taratibu halali za kupiga kura kwani chama kilichoko madarakani kinaweza kutumia kila mbinu kubaki madarakani. Pia msisahau shinikizo kutoka mataifa ya magharibi. Tayari BBC wako hewani KISUMU Kwamba wanamjenga RAILA au wameenda kumbomoa hilo wanajua wenyewe. Pia msisahau KTN TV ambao nao wametua KISUMU na kuwaacha NATION TV Nairobi pekee. Ni siri iliyo wazi kwamba NATION wanawaunga mkono viongozi wa upinde. Hakuna kosa kufanya hivyo, hata mimi kinadharia nafanya hivyo. Lakini kuzingatia uchafu wa siasa nimelazimika kuandika haya. Siyo kwamba nimechafuliwa. La hasha. Nasema itakavyokuwa. Wakati wa uchaguzi vyombo vya habari hutumika kuwahadaa wananchi. Tayari KANU wameanza kuitumia mbinu hiyo vilivyo. Ndio maana wakenya wengi walifurahi kusikia kwamba ndani ya KANU kuna upinzani. Viongozi wa upinde wakiongozwa na Raila Odinga walikuwa wamemkatalia MOI kuhusu uteuzi wake wa Kenyata kama mrithi wake. Kile ambacho hakikutegemewa KANU kikawa kimetokea. Upinzani ndani ya chama kilicho na njia zote halali na zisizo halali kubaki madarakani. Joto kubwa la mabadiliko ya kisiasa likasikika nchi nzima na hata nje ya nchi. Kwa mara ya kwanza mawaziri ndani ya serikali ya MOI wakatoa mawazo yao kinyume na MOI. Iliwabidi wafanye hivyo, kwani hata kama wasingefanya Moi angestaafu tu. Wenyewe hawataki kustaafu kwani muda ulioisha kikatiba ni wa rais na siyo mawaziri. Kuna kila sababu za kuwaona viongozi wa upinde kama watu waliochukua hatua za kulinda maslahi yao kuliko yale ya wananchi. Lakini kwenye kampeni hatutayasikia hayo. Wananchi tutaambiwa kwamba KANU ni hivi na vile na wao ndio watakaotuletea maendeleo kama mvua. Ikifikia hapo, ndio maana siwezi kuwa mwanachama wa chama chochote cha kisiasa.

Kwamba joto la mabadiliko ya kisiasa Kenya lililetwa na viongozi wa UPINDE hiyo siyo siri. Lakini muda waliopoteza wakisubiri kinyanganyiro cha KASARANI, umechangia kupunguza joto hilo. NAK walipomtaja mgombea wao KIBAKI, walikuwa tayari wamewaambia viongozi wa upinde waamue kusuka au kunyoa. Yaani waliwaambia kama mnataka kutoka KANU fanyeni hivyo haraka, ili msimamo wenu ujulikane mapema. Hawakufanya hivyo, na NAK hawakuwa na jingine ila kutangaza msimamo wao bila viongozi wa upinde. Kwa upande wao, viongozi wa upinde walikuwa wakisubiri KASARANI washindwe, ndipo wachukue hatua ya pili. Kweangu hilo ni kosa. Walitakiwa kusoma ishara za mwalimu wao MOI wajue kwamba hapa hakuna tumaini. Bila kupoteza wakati wangechukua hatua za haraka kuihama KANU. Kwamba walingojea mpaka dakika za mwisho, hiyo inaonyesha jinsi walivyoipenda KANU. Kama malengo yao yangetimia huko KANU ni dhahiri kwamba wasingetoka. Wametoka kwa sababu malengo yao hayakutimia. Je malengo yao yalikuwa yepi? Swali hilo ndilo wakenya wanasubiri majibu yake. Baada ya kuihama KANU dakika za mwisho, walijiunga na NAK. Wakapokelewa japo walikuwa wamechelewa. Kazi ambayo NAK walikuwa wamekwisha ifanya ikabidi wairudie kwani wageni wameingia. Nafasi ambazo walikwisha gawana, ikabidi wajadili tena jinsi ya kuwajumuisha wana upinde. KITENDAWILI KIKO HAPO. Hatujui walikubaliana vipi kuhusu nafasi za uongozi, lakini walisema kwamba KIBAKI atabaki katika nafasi ya urais. Tuombe iwe kwamba waliafikiana wote katika hilo.

Baada ya kusema hayo, niwapongeze kwa kila hatua wanayoichukua. Inawababaisha sana KANU. Inaonekana wote ni wanafunzi waliojifunza vizuri mbinu za kisiasa kutoka kwa Profesa MOI. Je wanafunzi humpita mwalimu wao? Kibiblia haiwezekani. Lakini kielimu na kisiasa inawezekana. Je siasa hufuata biblia ? Hapana. Wanasiasa hutumia dini kutawala, lakini hawataki watu wa dini wahusike katika kutawala. Husema kwamba serikali haina dini, lakini watu ndani ya serikali wana dini zao ambazo siyo muhimu sana kwa serikali.Watu wa dini hutawaliwa na serikali wakati Mungu wanayemwabudu ni mkuu kuliko serikali. Nataka kuibadili hali hiyo. Lazima tutengane. Watu wa dini wakome kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.Wanasiasa waendeshe siasa wakiwatumia watu wasio na dini yeyote. Wakiunda serikali na waseme serikali haina dini., hapo watakuwa wamesema kweli. Lakini mambo yalivyo sasa wakisema kwamba serikali haina dini, wanatudanganya.


Taarifa ya HABARI

Baada ya Kibaki kuchukua hatamu za uongozi Kenya, Ahadi nyingi walizoahidi wakati wa kampeni bado hawajatimiza. Katiba waliyoahidi kuibadili siku mia moja za kwanza mdarakani, bado haijakuwa tayari. Kila dalili zinaonyesha kwamba Kibaki hataki katiba mpya itakayompunguzia madaraka. Tunachokishuhudia sasa ni kamati za kuchunguza kamati itakayochunguza kama katiba mpya inatakiwa. Wengi wanaliona hilo kama kupoteza muda wakati nia ya kuweka katiba mpya haiko kwa Kibaki. Wanasema hiyo ndiyo siasa. Kudanganyana mchana kweupe, Jua likiwaka?

Vyama 15 ambavyo ndivyo vinavyojumuisha muungano wa Narc National Reimbow coalition, vilikutana chini ya uenyekiti wa rais Kibaki kujadili mzozo uliojitokeza katika chama hicho. Utata ulizuka pale wanachama wa muungano huo walipoambiwa kwamba wavifute vyama vyao na badala yake wajiunge na chama kimoja cha Narc ifikapo desember mwaka huu. Wengi walisema kwamba enzi ya chama kimoja ilipita kitambo, na kuwarudisha kwenye enzi hizo ni sawa na ndoto za mchana. Chama cha kwanza kupinga pendekezo hilo ni LDP. Walisema siku za kuongozwa kidicteta zilikwisha. Pia walisema kwamba hawakujiunga na Narc ili wamezwe bali kuunda muungano utakaolinda maslahi ya kila chama. Kwamba walisema Kibaki mwanachama wa DP anatosha, haikumaanisha wamezwe na DP kwa jina jipya la Narc. waliongeza kwamba Narc itabaki muungano wa vyama, na itakuwa imara kama makubaliano yaliyowaunganisha yatafuatwa. Vinginevyo walisema hapana hawatakubali. Nalo gazeti la NATION likiripoti habari hizi kwenye ukurasa wake wa mbele lilisema "Narc kuungana kama chama kimoja mwishoni mwa mwaka." Kwao hawakuziona tofauti zilizojitokeza mkutanoni, jambo linaloashiria kwamba gazeti hilo linaunga mkono vyama vingine kumezwa na DP kwa jina jipya la Narc. Ndiyo maana watu wengi siku hizi husoma Standars na Kenya Times kwa habari sahihi. Kwamba vyombo vya habari vitakubali kutumiwa kuturudisha kwenye utawala wa kiimla hilo linatisha. Redio injili Fm itasimamia haki daima. Usikose kuisikiliza kwa habari sahihi. unaendelea kuisikiliza taarifa ya habari kutoka redio injili fm, inayokutangazia ulimwenguni kote kwenye masafa ya Internet www.munishi .com/ redio injilifm

Wanasiasa huchaguliwa na wananchi ili waingie bungeni kutunga sheria. Wakisha fanya hivyo, Sheria inapaswa kuwa kama msumeno unaoweza kuwakata hata wanasiasa wenyewe. Inapotokea kwamba wanasiasa ndio wanaoongoza katika kuzivunja sheria, wanategemea nani katika jamii azitii sheria? Inasikitisha tunapowaona wanasiasa Afrika wakiunda kamati za kuwachunguza wafisadi katika taasisi mbalimbali, na wanasahau kuichunguza taasisi yao ya siasa ambayo imeoza kwa maovu ya kila aina. Kuanzia mauaji ya kisiasa ufisadi, Uongo ulio wazi, pamoja na unafiki. Wanapambana na ufisadi siyo kwa sababu wanauchukia, bali wanafanya hivyo baada ya kuwekewa shinikizo na mataifa ya magharibi na hasa Amerika. Ndio maana ufisadi kumalizika Afrika ni sawa na ndoto za mchana. Wanaojaribu kupambana na ufisadi wanafanya hivyo baada ya kuamrishwa na Amerika ambao nao ni wafisadi nambari moja. Waamerika wakitaka kuanzisha chochote katika nchi za wenyewe, wako tayari kutoa chochote ili wafanikiwe. Je huo siyo ufisadi? Nchini Tanzania wamenunua kila kitu. Wanatumia lugha ya ubinafsishaji kufanikisha malengo yao. Mashirika yote ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi Afrika yako mikononi mwa makampuni ya nchi za magharibi na Amerika ndiyo inayoongoza katika hilo. Inatia kichefuchefu tunapowasikia viongozi Afrika wakiwasha moto wa mabua kupambana na ufisadi kiunafiki. Moto wa namna hiyo huzimika mara wanapopewa walichoahidiwa. Wakati umefika kwa viongozi wa kidini kuunda kamati za kuwachunguza viongozi Afrika. Wawafundishe kuzichukia dhambi kwa dhati, na wapambane nazo kwa sababu wanazichukia na siyo unafiki wa kushinikizwa na ahadi za misaada kutoka Amerika. Kinyume cha hayo, wasitegemee kwamba kuna mtu atakayetii sheria ambazo wenyewe wanazivunja. Ikiwa wanasiasa wanawezakubaliana jambo mbele ya mwanasheria, halafu baadaye wakiuke makubaliano, Mnategemea wanasheria kuheshimu sheria? Ndio maana vyombo vya sheria haviheshimu sheria. Siasa inapokuwa sheria, na sheria kuwa siasa wananchi tuko hatarini. Nasikitika kusema kwamba katika nchi zetu za Kiafrika kila kitu ni siasa na siasa ni kila kitu. Ndiyo maana hatua za haraka lazima zichukuliwe kutenganisha siasa na maisha yetu. Tuwe na mahali pa kumuomba Mungu na kuzitii sheria zake bila siasa. Rais anapotumia nguvu za katiba ya zamani kuwasimamisha kazi majaji waliomwapisha aingie ofisini, ni wakati wa majaji hao kumkumbusha kwamba aliahidi kuweka katiba mpya baada ya siku mia moja. Wakishindwa kumuuliza, waombe msaada wa maaskofu, waunde kamati ya kumchunguza.

Kamati zimekuwa nyingi, na kinachohitajika sasa ni kamati za kuchunguza kamati. Kabla ya kamati za kuchunguza kamati kuundwa, msisahau kuunda kamati ya kuvichunguza vyombo vya habari. Mchango wao katika kuwasaidia wanasiasa kuendeleza maovu katika jamii. Kamati zitakapokuwa nyingi, itabidi na zenyewe zichunguzwe na kamati zitakazopeleka ripoti kwa kamati zinazochunguza kamati. Majaji wanaosemekana wafisadi, waliwahi kuwahukumu wengi waende jela, na wengine walihukumiwa vifo. Kwa kuwa imegundulika walikuwa wafisadi kesi walizohukumu awali zitarudiwa ili haki itendeke? Mtafanyaje na wale waliohukumiwa kifo na majaji hao? Huwezi kuisafisha bahari kabla ya kusafisha mito michafu inayoleta maji baharini. Kufanya hivyo ni sawa na kujaribu kuukimbiza upepo. Wanasiasa waache kutudanganya. Wao ndio wamehujumu uchumi. Wakirudisha pesa zote walizojipatia kwa njia za ufisadi, uchumi utarekebika ili watumishi wa umma wapewe mishahara ya kuwatosha. Ni kweli kwamba hakuna pesa zinazoweza kumtosha mwanadamu, lakini angalau mishahara yao itoshe kumudu maisha ya kila siku. Ikiwa mishahara haitoshi chakula, mnategemea nini kutoka kwa watumishi kama hao? Rushwa ni mbaya na siwezi kuwatetea wafisadi. Lakini wafisadi hawawezi kuumaliza ufisadi. Kupambana na ufisadi ni hatua nzuri. Kufanya hivyo ili kuwaridhisha Amerika wafisadi mambari moja, ni vibaya sana. Hatua nzuri ikichukuliwa kwa lengo baya, inaharibu kila kitu. Mwisho hata hatua yenyewe inakuwa mbovu.

Wito umetolewa kwa viongozi Afrika kuimarisha huduma za afya nchini mwao. Gharama za matibabu katika bara letu ni za juu kiasi kwamba wananchi wengi wanashindwa kumudu. Viongozi Afrika hawafanyi juhudi kuboresha mahospitali badala yake hujilimbikizia pesa za kutibiwa ngambo endapo wataugua. Pamoja na jitihada za viongozi wengi Afrika kujipenda kuliko wananchi wanaowaongoza, Wengi walioenda kupata matibabu ngambo walirudi maiti. Nyerere na Mobutu ni mfano wa viongozi waliotumia pesa nyingi kutibiwa nje ya Afrika lakini bado mauti iliwaita. Kenyatta Rais wa kwanza Kenya alikataa kata kata kupelekwa ngambo kutibiwa. Pamoja na mambo mengine hakuwaamini madaktari wa nchi za magharibi. Alihoji kama watu wametutawala na wameondoka shingo upande, nini kitawazuia kummalizia kiongozi mgonjwa wa bara hili wakati atakapokataa kusaini mkataba wa kuyauza mashirika yetu kwa makampuni yao ili waendelee kutunyonya? Aliongeza kwamba wakoloni watautumia ugonjwa wa kiongozi wetu kama mtego wa kunasa panya. Siyo ajabu akaambiwa auze sehemu ya nchi iwe kambi za kijeshi za taifa linalompa matibabu. Wananchi wengi Afrika walimpenda Kenyatta kwa msimamo huo. Aliwaamini madaktari wa kiafrika, na alifanya kila juhudi kuwasomesha ili waitumie taaluma yao barani Afrika. Leo hii madaktari wetu wanaikimbia Afrika kulipwa pesa nyingi nchi za magharibi. Kwao pamoja na viongozi wanaojipenda, tunasema AIBU KWENU. Wananchi tunasema Mungu atatusaidia. Imani yetu kwake itatuponya hata kama tutatafuna majani ya miti kama dawa. Anayaona mateso yetu, na anaona jinsi viongozi wanavyojipenda wenyewe. Atahakikisha kwamba wakienda ngambo kutibiwa wakiwa moto, watarudi Afrika wakiwa baridi. Lakini wakitaka laana hii iwaondokee, waanze sasa kuziipa kipau mbele huduma za afya katika nchi zao.
Kibaki akiapa kuiongoza Kenya baada ya kuingia madarakani kwa kishindo. KANU ilipata pigo ambalo isingekuwa rahisi kwao kuamka tena. Lakini mambo yalivyo sasa ni kwamba Kibaki anajichimbia kaburi kisiasa akijua au akiwa hajui.

Mmoja kati viongozi wa tume ya kurekebisha katiba, ameuawa kwa kupigwa risasi. Daktari Othiambo Mbai ambaye pia ni mkufunzi katika chuo kikuu cha Nairobi alishambuliwa nyumbani kwake na watu wenye silaha. Majirani walimkimbiza Nairobi Hospital ambako aliaga dunia alipokuwa akifanyiwa upasuaji kuondoa risasi nne mwilini mwake. Kulingana na madaktari waliomfanyia upasuaji, Daktari mbai alikuwa na majeraha ya risasi kichwani mkononi tumboni na kwenye paja. Inaonekana kwamba wauaji wake walikuwa wamekuja kufanya kazi moja tu. Nayo ni kumuua Daktari Othiambo Mbai. Akiongea na waandishi wa habari hospitalini, Mheshimiwa Raila Odinga alisema kwamba mauaji ya Daktari Mbai ni mauaji ya kisiasa. Naye Profesa Yash Pal Ghai alisema kwamba inaonekana kwamba wauaji walikuwa wamekodishwa kufanya kazi hiyo. Lakini naibu mkuu wa polisi Nairobi bwana Nicodemas Diffu alisema wanayachukulia mauaji hayo kama uhalifu wa kawaida mpaka ushahidi wa aina nyingine upatikane. Alipoulizwa kwamba waliupata wapi ushahidi kwamba hao walikuwa wahalifu wa kawaida alisema bado wanafanya uchunguzi.

Siasa ni siasa. Yaani kitu ambacho siyo chenyewe hasa. Ikiwa Mwanasiasa anaweza kumdanganya mwanasiasa mwenzake mchana jua linawaka, bila kujali kwamba makubaliano yao waliandikiana kwa wakili, vipi kuhusu ahadi walizotuahidi wananchi bila maandishi yeyote? Inapokuwa wazi kwamba wanasiasa wanaweza danganyana, ndipo wananchi tunapofunguka macho. Kwa vyovyote lazima tumuonee huruma aliyedanganywa hata kama kwa sasa hana la kufanya. Bila kujua, huyo aliyedanganya amejipunguzia heshima yake kisiasa na kidini. Alisaidiwa na sasa haoni kama alisaidiwa. Msemo wa kiswahili kwamba shukrani ya punda ni mateke sasa unamaanisha kwa wengi.

Yale yaliyotajajiwa na wengi, sasa yametimia. Imekuwa wazi kwamba viongozi walio madarakani hawana haraka ya kuirekebisha katiba. Wanadai kwamba ile ya zamani ndiyo waliyoaapa kuilinda na kuitetea. Mbaya zaidi wanasemea kanisani mahali ambapo ukweli ulipaswa kutiliwa maanani. Itakumbukwa kwamba wakati wa uchaguzi mkuu uliomalizika, ahadi nyingi zilitolewa na moja ikiwa ni kuhakikisha katiba mpya imeidhinishwa baada ya siku mia moja za uongozi mpya. Pamoja na mambo mengine katiba mpya ilipaswa kuwa na vipengele vinavyopunguza madaraka ya rais ili asiyatumie vibaya kama waliomtangulia. Na hapo ndipo suala la waziri mkuu lilipochipukia. Lakini mambo yalivyo sasa inaelekea kwamba harakati za ukombozi ndio kwanza zinaanza. Kwa wananchi mambo yanaelekea kuwa kama yalivyokuwa kama siyo mabaya zaidi ya ilivyokuwa. Ushwari wa kisiasa ulioonekana kipindi chote cha mwanzo umeanza kupata mbadala wake ambaye ni maandamano ya wanafunzi wanaobeba mabango yaliyoandikwa MoU yakimaanisha Memorandan of Understanding, au Makubaliano ya awali. Ilianzia kwenye mazishi ya Wamalwa ambapo Polisi wa kutuliza ghasia walikabiliana na wanafunzi hao vilivyo. Yote haya ni ya nini? Serikali ya haki, Polisi wake wa kutuliza ghasia wanakuwa kambini siku zote. Ukishaanza kuwaona mitaani na hata kwenye mazishi, ujue kuna majambo hayaendi vizuri na nguvu inatumika kunyamazisha mambo. Nguvu inaweza kunyamazisha jambo kwa muda, lakini haiwezi kulizuia lisitokee hata kama itachukua muda gani. KANU walitumia nguvu kupita kiasi kuzuia mabadiliko, lakini hatimaye yalitokea na sasa wako nje ya madaraka. Walioko madarakani wakisahau waanze kuyazuia mabadiliko yaliyotarajiwa yasitokee, watajikuta wakinyolewa na wembe walioutumia kuinyao KANU. Mungu ibariki Kenya. Bariki na Tanzania, Tena uisaidie nchi ya Tanzania iweze kuyafikia mabadiliko hatua ya kwanza kama yaliyotokea Kenya. Viongozi Kenya wasaidie wasijisahau mapema kutimiza ahadi walizowaahidi wananchi mbele yako. Uliwasikia wakiahidi na wasaidie wayatimize yote waliyoahidi ili Kenya iwe mfano mwema wa kuigwa Afrika.

Nairobi Ufisadi bado ni maji marefu yanayotishia kuzamisha wengi. Ila tunatoa pongezi zetu kwa viongozi wa serikali mpya kwani mabadiliko mengi yameanza kuonekana. Sasa unaweza kuhudumiwa katika ofisi za serikali bila kutoa kitu kidogo. Waliahidi kupigana na ufisadi na na matunda tumeanza kuyaona. Lakini haimaanishi kwamba ufisadi umeisha kabisa. Ndio maana siyo busara kupuuzia kelele zinazopigwa na baadhi ya viongozi kwamba dalili za ufisadi zimeanza kuonekana. Mtu msafi akionyeshwa doa kwenye nguo yake atafurahi ili aliondoe abaki msafi. Ila akibisha kwamba hakuna doa nasi tunaliona, basi yatakuja madoa mengi mpaka rangi ya nguo itapotelea kwenye madoa

Mtu akikosa adabu, Hafundishwi adabu kwa kukosewa adabu. Tena mtu akiiba, adhabu yake siyo kuibiwa. Mwizi anaweza kutuonyesha mwizi kwa sababu wanajuana. Mkisema yeye ni mwizi na hafai kuwaonyesha nani anayewaibia, Basi mtaibiwa sana. Na kitambo mjue kwamba mnaibiwa, mtakuwa mmechelewa sana. Waacheni watuambie nani anayetuibia, Kwani ni kosa kufikiri kwamba serikali mpya haiwezi kuwa na wezi wa mali za umma. Wengi walihusika na yote yaliyotufika katika serikali za awali. Nini kitawafanya wasiyarudie waliyoyazoea? Au walitubu? Sikuwasikia wakitubu, bali walihama kwenye jahazi lililokuwa likizama na wakajisalimisha kwenye meli ya Narc iliyokuwa inakaribia kungoa nanga. Kwangu niliwaona kama watu waliojisalimisha wenyewe wasizame siyo kwamba walikuja kutuokoa tusizame. Wananchi bado maji yako shingoni. Maisha bado ni magumu. Pesa hazipatikani kirahisi. Zikipatikana matumizi yake ni mengi wala hazitoshi. Kazi hakuna, Na vitambulisho vya wasio na kazi hawatoi. Kukosa kazi ni kosa la jinai na wengi wako ndani kwa kosa hilo. Tunaendelea kuzama na wenzetu wameokoa taaluma zao za kisiasa zilizokuwa hatarini kuzama. Tunainua mikono yetu watuone ili sasa waonyeshe kweli kama wanaweza kutuokoa. Njoni mtutoe kwenye dimbwi hili la umaskini. Ndiyo mnasema tufanye kazi kwa bidii sawa. Ziko wapi kazi zenyewe?

Sanaa na wasanii Imebainika kwamba wale wanaouza kanda bandia za muziki watachukuliwa hatua kali za kisheria watakapobainika. Hii ni kufuatia ongezeko la kutisha la wahuni wanaojihusisha na biashara haramu ya kuuza kanda bila kibali cha wasanii husika. Ni kutokana na hawa wanaouza kanda bandia, ndio maana kiwango cha muziki kimeshuka. Wasanii wengi wameshindwa kurudi studio kurekodi toleo jingine kutokana na wizi wanaofanyiwa mchana jua likiwaka. Ni matumaini yetu kwmba vyombo vinavyohusika vitaliangalia kwa makini suala hili. Wasanii wanaumia na kuteseka, huku wahuni wachache wakijitajirisha kwa jasho la wenzao. Tena kuna mtindo uliozuka siku hizi wa watu kujiita maprojusa, kumbe ni matapeli wanaowarubuni wasanii kwa pesa kidogo ili wapate haki ya kuuza kazi za wasanii hao bila kuwalipa ipasavyo. Inasikitisha kuona kwamba hata REDIO HABARI MAALUM inajihusisha na hujuma hizo.Inaweka gharama za kurekodi muziki katika redio yao ziwe kiwango cha juu sana. Wasanii wanaposhindwa kulipa gharama hizo, wanalazimishwa kuingia katika mikataba feki ya kiutapeli. Kabla wajue nini kinaendelea wanazikuta nyimbo zao zikiuzwa afrika ya mashariki na kati bila wao kupata chochote. Tunalaani wizi huu kwa nguvu zetu zote. Wakati umefika kwa wasanii hasa wa nyimbo za injili, wakatae kunyanyaswa na wasimamie haki zao. Wasipoamka hakuna mwingine wa kuwatetea kama si wao wenyewe.

Ukimwi na uchumi Afrika Nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na tishio la kuzorota kwa uchumi. Hii ni kutokana na vifo vingi vinavyotokea barani humo, na vingi vinahusishwa moja kwa moja na UKIMWI. Kulingana na mila na desturi za Kiafrika, mtu anapokufa, basi ndugu jamaa na marafiki huacha kila shughuli na kuanza maombolezo ya muda mrefu. Katika maombolezo kama hayo pesa nyingi hutumika kuwalisha waombolezaji, na ngombe kuku na mbuzi huchinjwa wakati wa maombolezo. Wadadisi wanasema kutokana na idadi kubwa ya vifo vinavyotokea siku hizi itabidi waafrika walitizame upya suala la maombolezo yenye gharama nyingi. Tuendako, Mbuzi,kuku na ngombe wa kuchinjwa watamalizika, na hatujui mazishi ya siku za usoni yatakuwa ya jinsi gani. ILa kutokana na dini ya kiislamu kuota mizizi Afrika, wengi wameanza kuzika kiislamu ambapo mtu akifa anazikwa mapema iwezekanavyo kuepusha gharama kubwa ya mazishi. Hata wakristo wengi wameanza kufuata mkondo huo kwani maji yakizidi unga hakuna jinsi. Wengi wanasema juhudi kubwa zinatakiwa zielekezwe katika kuwatibu na kuwaonyesha upendo wagonjwa wanapokuwa hai, badala ya kungoja waage dunia na kuanza unafiki wa kuomboleza kwa gharama za juu kuliko zilizotumika kuwatibu walipokuwa wagonjwa. Hata biblia inatufundisha kwamba ni afadhali mbwa mzee aliye hai, kuliko simba kijana aliyekufa. Mtu akiisha kufa, FAILI yake duniani na mbinguni inakuwa imefungwa. Haijalishi wanadamu watafanya nini, lakini haitabadili ukweli kwamba ameenda, nasi tunasubisi siku yetu ya kumfuata alikokwenda. Mtu akienda Amerika ni ajabu kubwa kwani wengi wetu huenda tusifike Amerika wakati wa uhai wetu. Lakini mtu akifa siyo ajabu kwani sote siku moja tutakufa.

Nalo neno la Mungu katika kitabu cha mithali 5:15-22 linasema ifuatavyo: Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako. Je! chemchemi zako zitawanyike mbali, na mito ya maji katika njia kuu? Yawe yako mwenyewe peke yako, Wala si ya wageni pamoja nawe. Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezae. Maziwa yake yakutoshe siku zote. Na kwa upendo wake ushangilie daima. Mwanangu mbona unashangilia malaya, na kukikumbatia kifua cha mgeni? Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya Bwana. Na mienendo yake yote huitafakari. Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake.

Dar es salaam Kanisa la Full Gospel Bible Felloship linaloongozwa na Kakobe limeitisha mkutano wa wachungaji wa kipentekoste Tanzania nzima. Lengo la mkutano huo imeelezwa kwamba ni kuweka mikakati ya kujenga mahusiano mazuri kati ya kanisa na serikali. Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti wa umoja huo Askofu Sylvester Gamanywa alisema, wakati umefika kwa serikali kutowapuuza wapentekoste. Alidai kwamba wapentekoste hawapewi nafasi katika vyombo vya habari vya kitaifa jambo ambalo alisema limechangiwa na dhana potovu kwamba walokole ni watu waliochanganyikiwa kimaisha na hawana lolote la kuweza kuisaidia serikali kiutawala. Naye Askofu Kitonga wa kanisa la Redeemed Kenya alisema anaunga mkono kongamano hilo na akasema anafurahi kuona askofu Kakobe akiufuata ushauri wake wa kutoipinga serikali iliyoko madarakani. Aliongeza kwamba nchini Kenya serikali iliyokuwa madarakani ilitambua umuhimu wa wapentekoste na iliwatumia sana katika kuwasilisha sera za serikali kwa wananchi ambao wengi ni washirika wa makanisa hayo. Lakini wale wanaopinga wazo la kanisa kununuliwa na serikali wanasema, Kanisa ni chombo cha kukemea maovu katika jamii na serikali ikiwa mojawapo. Waliongeza kwamba Kanisa linapokubali kununuliwa na serikali, hiyo ni hatari kubwa. Walisisitiza kwamba Inasikitisha kuona kwamba kanisa la Tanzania limekubali kununuliwa na serikali ya CCM ambayo sifa yake ni kuwaua raia wasiokubaliana na sera zao mbovu za wizi , Ukandamizaji, na uonevu wa kila namna kwa raia wa Tanzania. Mungu lisaidie kanisa lako Tanzania.

Nairobi Kufuatia kifo cha aliyekuwa makamu wa rais Mheshimiwa Maiko Wamalwa Kijana, upepo wa kisiasa nchini Kenya umebadili mkondo wake. Sasa kila sikio limeelekezwa kusikia nani atakayechaguliwa kushika nafasi ya makamu wa rais. Wengine wanasema lazima karata ya ukabila ifuatwe na makamu wa atoke Uluyani, na kuna wale wanaosema sasa ni wakati wa wa kuweka ukabila pembeni na kumchagua yeyote anayeweza kuishikilia nafasi hiyo hata kama hatoki Westani Kenya. Saitoti anaonekana na wengi kuwa na uzoevu wa kazi hiyo japo kuna dosari ndogo ndogo. Wengine wanasema kuwa Mudi Awori anafaa kikabila hata kama hana uzoevu. Wanadai kwamba mtu hawezi kuupata uzoevu kabla hajaanza kazi yenyewe.

Liberia Aliyekuwa rais wa Laiberia Charles Tailor amekubali kuihama nchi yake, ili akaishi uhamishoni nchini Nigeria. Hii ni kufuatia shinikizo alilowekewa na nchi za magharibi zikiongozwa na Amerika. Kwao Tailor akiondoka Liberia, matatizo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia yatakwisha. Swali ambalo wengi wanajiuliza ni kama Tailor ndiye aliyekuwa tatizo Liberia. Wachunguzi wa mambo wanadadisi kwamba Amerika ndio wamekuwa wakichochea vita katika nchi nyingi za kiafrika kwa lengo la kulinda maslahi yao katika bara hili. Tunasubiri kuona raia wa Liberia wakiishi kwa amani bila au na Tailor mradi tu yawe ni matakwa yao na siyo shinikizo kutoka Marekani.

Nairobi Mzozo mkubwa uliokikumba chama cha tawala Nack unatishia kukisambaratisha chama hicho kama hatua za haraka hazitachukuliwa kukinusuru chama. migawanyiko imejitokeza baada ya wanachama wa muungano huo kudai kwamba makubaliano yaliyowaleta pamoja yameanza kukiukwa. Suala lililozua utata zaidi ni lile la waziri mkuu nafasi aliyoahidiwa mheshimiwa Raila Odinga. Wengine wanasema hawakukubaliana hivyo, na kuna wale wanaokubali lakini wanasema waziri mkuu hatakiwi kuwa na uwezo kuliko rais. Hakuna atakayepinga kwamba tofauti hizo zimekitikisa chama cha Narck ambacho kiliingia mararakani kwa kishindo na kukitoa madarakani chama cha KANU ambacho mpaka sasa hakijayaamini macho yake kwamba kimewekwa benchi. Naye mbunge wa Nakuru akiwaonya wakereketwa wa nafasi ya waziri mkuu, alitoa maneno yenye cheche za moto pale alipowakumbusha kuhusu kuuawa kwa mwanasiasa mashuuri Tom Mboya. Alieleza sababu zake ambazo wengi wamezitafsiri kama matisho. Wengi wanajiuliza ikiwa Tom Mboya wakati wa Kenyatta na Ouko wakati wa Moi walikutana na vifo vyao katika mazingara ya kutatanisha, je nani anayeweza kufuatia? Mungu apishe mbali. Ni maombi yetu wakubaliane kutimiza makubaliano yao ya awali kuepusha shari. Mungu ibariki Kenya.

Makanisani Redio Biblia husema FM ambayo hutangaza katika megahads 90.9 katika viunga vya Nairobi na megahads 96.9 katika Machakos na mkoa wa kati sasa haiko hewani. Hii ni kufuatia msako uliofanywa na maofisa wa forodha katika kituo hicho na kungoa mitambo ya kurushia matangazo kwa kile walichokiita kwamba mitambo hiyo haijalipiwa ushuru. Japo mitambo midogo ya 90.9 Nairobi haikuchukuliwa, lakini ile iliyokuwa ikiwawezesha kusikika mkoa wa kati na bonde la ufa yaani Nakuru Eldoret hadi Bungoma Imezimwa. Hii ni stesheni ya kwanza kuzimiwa mitambo yake ya kurusha matangazo tangu kuundwa kwa serikali mpya. Wakati wa serikali ya zamani, Redio CITIZEN na TV yao ndiyo ilikuwa ikifungiwa kila kukicha. Lakini sasa ndio wanaotamba kila kona ya nchi. Redio CITIZEN Bila kuona haya, wakati wa uchaguzi mkuu walikipigia debe chama cha Narc na kazi yao ilizaa matunda pale Narc iliposhinda kwa kishindo na kuunda serikali mpya. Wakati huo ilisifika kwa kuikosoa serikali, na sasa inasifika kwa kuisifia serikali. Wengi wanajiuliza kama sasa ni zamu ya Redio ya injili Biblia husema FM kuzimiwa mitambo yao kama CITIZEN wakati huo? Tunaomba isiwe hivyo. Hasa wakati huu ambao serikali inaweka huru masafa ya kutangaza. Ni matumaini yetu kwamba vyombo vya habari vitakuwa huru kuliko mwanzoni, lakini siyo kwa ishara tunazoanza kuziona. Mkurugenzi wa redio hiyo amesema kwamba walipewa barua ya kuwawezesha kukwepa kulipa kodi kwani redio yao ni chombo cha kuhubiria Injili na wala siyo kwa ajili ya biashara. Redio hiyo inamilikiwa na kanisa la AIC ambalo rais mstaafu Daniel Arap Moi ni mshirika wake. Rais aliyeko madarakani kwa sasa ni mshirika wa kanisa katoliki na tayari kanisa hilo lina redio yenye mitambo ya nguvu. Yao haijazimwa, kwa nini wengine wazimiwe. Hayo ndiyo maswali ya walio wengi.

Amerika Makanisa ulimwenguni yamegawanyika kuhusu suala la kutawazwa uaskofu askofu shoga wa kimarekani. Kwa mara ya kwanza Amerika inataka kutumia nguvu yake ya kushawishi duniani ili dunia ikubaliane na ushoga, na sasa wanataka ikubaliwe kanisani. Tunawaunga mkono wote wanaoupinga uovu huu kwa nguvu zao zote. Na hii inathibitisha kwa mara nyingine kwamba Amerika siyo wakristo kama wanavyotutaka tuamini. Mmomonyoko wa maadili duniani umesababishwa zaidi na Amerika wakitumia sana vyombo vya habari na sanaa ya filamu zao chafu, na sasa wanataka kulitumia kanisa kusambaza uchafu wao kwa kisingizio cha uhuru wa kuamua. Tunasubiri kusikia misimamo ya makanisa kuhusu suala hili.


Lucy kiboko yao

Mama Lucy Kibaki akifoka alipokuwa ameweka kambi makao makuu ya gazeti la Nation.

Alidai kukasirishwa na taarifa za gazeti hilo kwamba alikuwa amevuruga pati ya aliyekuwa mkuu wa benki ya dunia. Kasheshe hilo lilidaiwa kutokea Muthaiga ambapo Mama Lucy Kibaki ana nyumba. Iliripotiwa kwamba jirani wa Lucy alikuwa na pati ya kumuaga, na ndipo Lucy ambaye hakualikwa kwenye pati hiyo, alipodai kwamba kelele za muziki zilikuwa zikimnyima usingizi.

Magazeti pia yalikuwa yameripoti kwamba mke huyo wa kwanza wa rais Kibaki alikuwa ameenda polisi mara kadhaa kuwataka wamkamate jirani wake huyo bila mafanikio. Ndipo Luvcy alipoamua kwenda mwenyewe kwa jirani huyo na kunyofoa nyaya za vipaza sauti, jambo lililowaacha wageni waalikwa midomo wazi kwa mshangao.

Pia magazeti hayo yalikuwa yameripoti kwamba mama huyo mtu mzima tena mke wa Rais, alikuwa ameingia kwa jirani wake akiwa na nguo za kulala. Pia iligundulika kwamba jumba hilo ni mali ya Kibaki na alikuwa amelikodisha kwa jirani wake huyo. Wengi waliona hilo kama usumbufu wa wenye majumba ya kupangisha ambao huwawekea wapangaji sheria chungu nzima. Kama hiyo haikutosha, mama huyo alidaiwa kuvamia jumba la Nation na kutaka ajulishwe nani aliyekuwa ameandika habari kuhusu UVAMIZI WAKE KWA JIRANI YAKE. Kilichowashangaza Nation ni kwamba Lucy wakati wote wa uvamizi wake hapo alikuwa amebeba gazeti la Standard maadui wao wa jadi. Japo mama huyo aliahidi kuwavamia Standard na KTN, ndoto yake hiyo haikutimizwa.

Haki ya magazeti kuandika, inaishia pale haki ya Lucy kupinga inapoanzia. Tena haki ya Lucy kulala usingizi inaishia pale haki ya jirani yake kusheherekea inapoanzia.

Baada ya kurupushani za shati kuchanika zilizochukua masaa matano Nation, Mama huyo aliondoka. Lakini siyo kabla ya kuwazaba makofi waliojaribu kumchukua picha akiwa katika oparesheni yake hiyo. Inasemekana kwamba alimdaka mpiga picha mmoja wa KTN na kumzaba vibao vilivyopelekea kamera yake kudondoka. Akifikiri yameisha, aliinama kuokota kamera akakutana na kibao kingine huku akiamriwa asalimishe mkanda wa picha kwa Bi Lucy. Mpiga picha huyo alikataa kuisalimisha kanda hiyo jambo lilichochea kipigo zaidi. Hatimaye alifanikiwa kubaki na kanda hiyo ya UVAMIZI WA LUCY NATION, ambayo baadaye aliiuza kwa vyombo vya habari ambavyo vilianza mara moja kurusha hewani Afrika mashariki na ulimwenguni kwa ujumla, jambo ambalo limeikera serikali.

Bwana Clifford Derrik mpiga picha wa KTN

Ilitazamiwa kwamba serikali ingetoa tamko rasmi baada ya tukio hilo, lakini mpaka sasa ni KIMYAA. Gazeti la Standard limeanza minongono kwamba mwandishi aliyeumizwa kazini atachukua hatua za kisheria kwani Lucy alivunja sheria kuvamia eneo la biashara na kujeruhi pamoja na kuharibu mali.Standard walisema kwamba kikatiba Lucy hayuko juu ya sheria na wala halindwi na mamlaka ya Rais. Wengine hasa wabunge wameanza kusema wanataka wakenya wafafanuliwe nini mamlaka ya mke au wake za Rais. Pia kumekuwepo na tetesi kwamba Kibaki ana wake wawili jambo ambalo Kibaki alikana hadharani. Bi WAMBOI ambaye anadaiwa kuwa mke wa pili wa Rais analindwa na walinzi kutoka serikalini, na isitoshe magazeti yamekuwa yakiripoti mengi afanyayo Bi Wamboi jambo ambalo halimfurahishi sana Lucy.

Kwamba ni tukio la pati kwa jirani ndilo lililozusha yote haya, tunasubiri tuone. Wadadisi wanaona vianzio vyote ni Media kujaribu kumpendelea Bi Wamboi na kumpa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari badala ya Mke wa kwanza wa Rais.Wengine wanaona Lucy ana haki za kutetea haki yake kama mke wa kwanza wa Kibaki. Ila kuna wale wanaokubaliana na hoja kwamba hata Wamboi apewe haki sawa na Lucy. Haijalishi tuna maoni gani, lakini mpira utabaki kwa Kibaki kwani yeye ndiye anayejua uhusiano wake na Wamboi pamoja na Lucy ulikuwa wa namna gani.


Lucy Kibaki akieleza malalamiko yake Nation huku akiwa amebeba gazeti la Standard. Sisi tunawauliza NATION na STANDARD Mbona mnamkasirisha Mama??

Vyombo vya Habari Kenya vimekiona cha mtema kuni vilivyojaribu kutoka katika mifuko ya wanasiasa ambamo vimekaa kwa muda mrefu. Kama kuonyesha kwamba wamenunuliwa, Lucy Kibaki mke wa rais wa Kenya, aliingia katika jumba la Nation bila woga kwani kwake hilo jumba pamoja na waandishi ndani yake ni mali yake. Anawalipa wasiandike mabaya yake wala mumewe, na alishangaa kuona wamekiuka maagano. Watamsema sana mama Lucy, lakini ukweli unabaki kwamba amewasaidia kuuza magazeti ambayo watu walikuwa wameyasahau kama bado yako. Lucy alivilaumu vyombo vya habari kwamba vinamdhalilisha mumewe. Alisema kwamba badala vimwite mumewe MTUKUFU RAIS KIBAKI, vimekuwa vikimwita "Kibaki" kana kwamba bado yuko upinzani. Kulingana na Lucy wanaotakiwa kudhalilishwa ni wapinzani.

Baada ya yote kusemwa na kutendwa, hatujui kama uhusiano wa vyombo vya habari na serikali utarudi ulivyokuwa tena. Inasemekana Lucy ana ushawishi mkubwa serikalini. Tayari mipango imeanza ya kukata makali ya vyombo vya habari. Kwa upande wake Media nao wameanza kuchora katuni za kashfa kwa Lucy. Tunasubiri kuona sitisho la mapambano, lakini jambo moja ni dhahiri. MAPAMBANO YAMEANZA.

Bwana Clifford Derrik mpiga picha wa KTN ambaye anadai kuumizwa akiwa kazini na camera yake kuharibiwa.Tayari amewasilisha malalamiko yake Kortini. Anasema hiyo ndio njia pekee ambayo anadhani haki itatendeka. Anadai alipigwa na kuumizwa mbele ya Polisi ambao hawakuchukua hatua yeyote. Pia anasema amekwisha ripoti makao makuu ya Polisi na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya Bi Lucy Kibaki, mke wa Rais wa Kenya.

"Kumbe mwandishi habari mmoja anaweza kuzua BONGE la "Story" ikagonga vichwa vya habari ulimwenguni!! Gazeti la Injili linawaomba pande zote wamalize mzozo huu haraka iwezekanavyo."
Hakuna sababu ya kijana kusimama Kortini na Mama yake. Na Mama kama amemchapa mtoto bila sababu na kuharibu camera yake basi amwite kama mtoto na amnunulie camera nyingine, halafu ampikie mwanawe chakula kizuri wale wafurahi, kisha waombane msamaha, YAISHE. Tunajua uwezo alio nao Mama Lucy, kwamba Serikali inaweza kuingilia kati na kufuta kesi, lakini yote hayo ni ya nini? Kutabaki kidonda cha mmoja kudhania kwamba hakutendewa haki. Tunasubiri busara za Mama zifanye kazi hapa." Pastor Munishi.


Contact us/ Tuandikie

Full Name
E-mail
Subject
Message
   
   

Tangaza Biashara yako Bure
Tuma picha na maelezo kwa munishi@munishi.com

http://munishi.com
FREE!

Send photo and information to munishi@munishi.com

Bonyeza hapa usome zaidi

Nyerere Msingi aloujenga Tanzania haufai, Tuubomoe.
Ujamaa ulishindwa, kwani CCM alioanzisha Nyerere sasa imezeeka. Sera zake zimeiharibu nchi yetu Tanzania. Tunataka mapinduzi tuitoe CCM madarakani ili tusinyanyaswe tena. Tumeonewa vya kutosha. sasa basi. CCM hatuitaki, imetufika shingoni. Tutaitapika.Mungu bariki Watanzania, wape hekima ya kutosha kuiweka CCM kapuni. Chukua usukani sasa kuiongoza Tanzania kwani kwa kipindi kirefu nchi yetu iliwekwa wakfu kwa shetani mpinzani wako. Tunamkataa shetani na CCM chama anachotumia kuwatesa watanzania, na tunaiweka nchi yetu mikononi mwako. Tumeomba machache hayo katika jina la Yesu Mwokozi wetu. Amen HABARI ZAIDI

 
| http://munishi.netfirms.com |