Munishi
Group:
Members Posts: 77 Joined: Nov. 2003
|
 |
Posted: Dec. 06 2003,16:25 |
 |
HISTORIA YANGU
INAENDELEA
Mpaka mwaka 1980 wakati nilipoamua kumpa Yesu
maisha yangu na kuokoka, Au tuseme nilizaliwa mara ya pili, Lakini
bado nilikuwa nikifanya kazi yangu ya kuandika nikitumia mashine.
Baada ya kuokoka, Na hii ilitokea mjini Arusha., Niliongeza ujuzi
katika kazi yangu. Pamoja na Machine za kuandika, pia nilianza
uchoraji kwa kutumia brashi na rangi. Sasa ikawa kwamba naweza
kuandika vibao vya matangazo ya biashara mbali mbali, Pia
nikajiongezea ujuzi wa kuandika hata kwenye nguo. Usisahau kwamba
hata vioo vya magari nilikuwa nimejipatia ujuzi wa kuviandika
nikitumia kipande cha almasi au wakati mwingine natumia machine ya
kupuliza rangi. Badala ya rangi, mimi nilikuwa naweka mchanga usio
na mawe. Mchanga ukipulizwa na mashine halafu uingie kwenye karatasi
iliyoandikwa na sehemu za herufi kukatwa na kubakiza mashimo ndani
ya herufi, basi zile herufi zinabaki kwenye kioo cha gari na nambari
ya gari inakuwa imechapishwa kwenye vioo vya pande zote. Ni miaka
zaidi ya ishirini lakini hata leo watu wanaandikiwa vioo vya magari
yao. Haimalizi wizi wa vioo, lakini inapunguza kwa kiasi kikubwa.
Mwizi hawezi kupoteza muda wake aibe kitu ambacho kitamwia vigumu
kukiuza. Na vioo vilivyoandikwa ni mojawapo ya vile vitu ambayo
mwizi hataki kuiba. Hata kama kuna uwezekano wa kufuta, Wezi
hawataki kazi nyingine baada ya kuiba. Wanataka wauze haraka
walichoiba wapate pesa ambazo ndizo lengo lao.
Pia mimi
ndiye wa kwanza kuwashawishi waalimu wa shule za msingi Dar kuandika
majina ya shule zao kwenye nguo za wanafunzi. Wakati huo shule zote
Dar zilikuwa na sare moja. Bluu na nyeupe. Usingeweza kutofautisha
huyu ni mwanafunzi kutoka shule gani. Haraka wazo likanijia, na
nikaanza kwenye shule ya msingi GEREZANI kuuza mawazo yangu kwa
mwalimu mkuu. Mawazo yangu yalinunuliwa jumla na nikaanza kuandika
mashati ya wanafunzi wote shuleni hapo. Tulikubaliana kwamba kila
shati litaandikwa kwa shilingi tatu, Na shilingi moja itabaki katika
mfuko wa shule na mimi nitachukua shilingi mbili kila shati. Baada
ya kumaliza shule ya kwanza, Nyingine zilifuata.
Ukizingatia
kwamba sasa mimi nimeokoka, Anasa na matumizi yasiyo na maana
niliyapunguza kabisa, Wakati huo nilipata pesa nyingi mpaka
zikaniwezesha kununua chombo cha MUZIKI kwa jina la ACCORDION. Kila
baada ya kazi nilikuwa nikijiunga na waumini wenzangu katika kwaya
ya kanisa. Chombo cha muziki kilikuwa kimoja tu na tuliotaka
kujifunza kukitumia tulikuwa wengi. Ni kutokana na hali hiyo ndipo
nilipoamua kununua chombo binafsi niweze kujifunza. Hamu yangu na
nia ya kutaka kujua kilichonivutia, Ilinifanya nielewe haraka
kucheza chombo hicho, baada ya maelekezo ya msingi. Ilikuwa silali
mpaka nijue kitu kipya katika MUZIKI. Wenzangu walishangaa kuona
tayari nimeanza kutunga nyimbo na kuziimba kanisani. Wengi
walivutiwa, Lakini Ernesti Milinga alivutiwa zaidi. Alikuwa mpiga
picha wa gazeti la DAILY NEWS. Aliponiona nikifanya kile
nilichokijua zaidi wakati huo, Yaani kuvuta accordion na kuimba,
Mzee milinga alivutiwa sana. Alitaka kuwa na mkutano na mimi, na
akaniambia angependa kuniendeleza zaidi KIMUZIKI. Alisema
kulingana na kipawa changu cha kutunga na kuimba, ingekuwa bora
nisomee lugha ya muziki ili niweze kuuandika na wengine wasome.
Alidai kile nilichokuwa nakijua wakati huo ni ni kucheza muziki
lakini singeweza kuuandika. Alijitolea kunilipia shule ya MUZIKI
BAMUTA. Nilisoma tangu mwaka 1982 mpaka mwaka 1983. Nayakumbuka
maneno ya Mzee Ernesti Milinga kwamba nikimaliza shule ya muziki,
halafu nichanganye na kipawa changu cha kutunga na kuimba, nitakuwa
nikijifunga tai mbili. Moja nitaifunga shingoni kifuani na nyingine
nitaifunga shingoni iangukie mgongoni. Wakati huo sikumuelewa,
lakini siku tulipokutana nikamuonyesha gari yangu niliyoinunua kwa
pesa za Muziki aliniuliza kama nayakumbuka maneno
yake.
Nimetunga nyimbo nyingi na zote zinapendwa na watu
wote. Kaseti yangu ya kwanza niliitunga mwaka 1980 lakini ilitoka
miaka sita baadaye. Hii ni kutokana na ukosefu wa pesa za kulipia
gharama za studio. Baada ya kuirekodi kanda yangu ya kwanza "FASHIO
NI YESU" mwaka 1986, ilifuatiwa na toleo la pili "NIKO CHINI
YA MWAMBA" Mwaka 1989 nilifunga pingu za maisha na mpenzi wangu
Prisca Munishi ambaye kwa pamoja tuliimba kaseti yetu toleo la tatu
PAKA AKILIA USIKU WENGINE HUSEMA WAMELOGWA. Kwenye kasha la kanda
hiyo hujulikana kama "YESU NA WEWE" Kwa sasa tuna watoto
watatu. Mojashi ndiye wa kwanza kuzaliwa mwaka 1990 akafuatiwa na
Salelo aliyezaliwa mwaka 1995 na mtopto wetu wa mwisho kwa jina la
MANGI alizaliwa mwaka 2000. Kisha baadaye nilitoa toleo
la nne "MAKOSA NI KOSA" mwaka 1992 na mwaka 1993 nikatoa toleo la
tano kwa jina UTAJAZA MWENYEWE. Mwaka 1995 nilitoa kaseti yangu ya
sita kwa jina "NAMLILIA MALEBO." Mwaka 2000 ndipo nilipotoa
kaseti yangu ya saba kwa jina "MPENDE ADUI." Ndani ya kanda hiyo
ndiko kuna maneno " CCM alianzisha Nyerere na sasa imezeeka. Sera
zake zimeharibu nchi yetu Tanzaniana na msiirudishe CCM madarakani."
Maneno hayo ndiyo yaliyoikasirisha serikali ya Tanzania inayoongozwa
na Mkapa, na kupelekea serikali kuifungia kanda hiyo.
 Kitambulisho
cha uanafunzi wa MUZIKI BAMUTA Ukiangalia usoni bado alama
nilikuwa nazo. Alama zangu nilizipata nikiwa na siku nne baada ya
kuzaliwa. Mama anasema kwamba nilikuwa nimelazwa kwenye nyumba ya
kienyeji ya KICHAGGA ambapo Ngombe na mbuzi pamoja na kuku walikuwa
na vyumba vyao ndani ya hiyo nyumba. Siku moja nikiwa nimelazwa
karibu na ukuta, Paka alimuona panya ukutani. Aliruka na kucha zake
tayari kumnasa panya na moja ya kucha zake zikanipitia usoni. Ndivyo
mama mzazi alivyoniambia. Nilijikuta na alama hiyo usoni ndipo
niliuliza. |