Munishi
Group:
Members Posts: 77 Joined: Nov. 2003
|
 |
Posted: Nov. 24 2003,12:33 |
 |

NYUMBANI NI NYUMBANI
http://munishi.com/
Pamoja na
kwamba unaweza kupata mali na utajiri ugenini, lakini huwezi kupata
kila kitu ugenini. Ndio maana Nyumbani ni nyumbani hata kukiwaje.
Sera zangu kuhusu Watanzania walio nje, ni kuwaomba warudi nyumbani
tuijenge Tanzania. Hata ukiwa na nini ugenini huwezi kuthaminiwa
kama ukiwa nyumbani. Kuna mengi ugenini ambayo kila kukicha
yatakukera. Swali kwamba utarudi lini kwenu, ni mojawapo ya mambo
yanayokera. Hata ukipewa uraia wa kujiandikisha, huwezi kupewa uzito
sawa na wazawa wa huko. Ombi langu kwenu Watanzania mlio nje:
Karibuni nyumbani kwani CCM iliyoharibu nchi mwisho wake umefika.
Leteni mali zenu na hakuna atakayewasumbua. Tutawapa nafasi za
kwanza za uwekezaji katika nchi yetu.
Mimi mwenyewe nimekaa
ugenini kwa muda mrefu. Japo ni taifa jirani ambalo hatupitani sana
katika mila na utamaduni, hukosi ya kukukera kama mgeni. Mfano
niliwahi kushinda nishani ya mwanzilishi wa kuimba nyimbo za injili
(SOLO) Lakini kwa sababu sikuwa raia, vyombo vya habari vilisema
kwamba nishani hiyo apewe mzawa. Wakampa nishani kwa sababu ni mzawa
lakini mwanzilishi ni mimi. Vitu vidogodogo kama hivyo
vinakukumbusha nyumbani.
Pamoja na kwamba Mkapa na CCM
walikuwa wameniwekea ukuta nisikanyage Tanzania, mwenyewe niliamua
liwalo na liwe na nikarudi nyumbani.Nilifurahi sana kuwaona wazazi,
ndugu na jamaa zangu ambayo zaidi ya miaka kumi tulikuwa
hatujaonana. Japo nilifuatwa kila nilikoenda na watu tofauti,
haikuniondolea furaha yangu ya kuwa nyumbani. Sitaki kuongeza chumvi
niseme kwamba nilikamatwa na kusumbuliwa, lakini nyendo zangu zote
zilifuatiliwa.
Kilichonihuzunisha ni habari za kukamatwa kwa
wenye maduka ya kanda za muziki. Kosa lao lilikuwa kuuza kanda ya
Munishi toleo la saba kwa jina "MPENDE ADUI" Ilidaiwa kwamba ndani
ya kanda hiyo kulikuwa na maneno "CCM aliyoanzisha Nyerere, Sasa
imezeeka. Sera zake zimeiharibu Tanzania, Na Ujamaa ulishindwa
kabisa, Watanzania Msiirudishe CCM madarakani." Hayo ndiyo maneno
yaliyodaiwa kuwa ya "UHAINI." Wenye maduka nchi nzima
waliwekwa ndani kwa kile kilichodaiwa "AMRI KUTOKA JUU" Wengine
waliachiliwa baada ya kukaa mwezi kwenye CELL za polisi bila
kufikishwa mahakamani. Wengine walitoa rushwa ya malaki ya shilingi
za kitanzania kununua uhuru wao. Wengine walionywa vikali kutouza
kanda zozote alizoimba Mwinjilisti Munishi.

Hii ndiyo
kanda ambayo Serikali ya CCM iliipiga marufuku
Mjini Moshi
mkoani Kilimanjaro, kuna mama mmoja ambaye sakata hiyo haikumwendea
vizuri na hivi tunapozungumza ni marehemu. Walikuwa wakimwita Mama
Tony, mkazi wa Kindi chini Muyuni kilomita mbili kutoka
sekondari ya wasichana "WERUWERU." Bila kujua kwamba kanda ya
Munishi imepigwa marufuku na serikali, yeye alikuwa akiziuza kwenye
duka lake lililoko soko kuu la Moshi. Duka lake liko kwenye mlango
wa kuingilia sokoni, na pengine ndiyo sababu likawa
maarufu.
Ilifika siku ya siku, ambapo maofisa kutoka kituo
cha polisi Moshi wealifika dukani kwake wakiwa wamevalia kiraia.
Waliikuta kanda hiyo inaimba kwani ilikuwa haibanduki kwenye kinanda
hasa ikizingatiwa kwamba ndiyo kwanza ilikuwa imetoka jikoni na
ilikuwa inauza kama keki moto. Maofisa walijifanya kana kwamba
hawaijui kanda yenyewe na wakauliza wapewe kanda ya Munishi kwa jina
Mpende Adui. Walipopewa moja, walisema kwamba waongezewe tatu kwani
walikuwa wanne. Baada ya kupewa walidai risiti na wakalipa pesa.
Kilichofuatia hata wewe unakijua.
Walimuamrisha huyo mama
kufunga duka, na wakaandamana naye kituoni. Alishinda huko mchana
kutwa, na usiku wake wakaandamana naye nyumbani kwake kufanya
upekuzi bila kibali kutoka mahakamani. Hawakupata walichokitafuta,
kwani kanda zote zilikuwa dukani, na tayari walikuwa wamezibeba.
Chini ya godoro walikuta pesa taslimu milioni tano za kitanzania.
Waliuliza kwa nini pesa kiasi hicho ziko nyumbani na siyo benki?
Majibu waliyoyapata yaliwasisimua zaidi. Mama Tony aliwajibu kwamba
mume wake yuko Mererani kwenye machimbo ya dhahabu na kwamba shimo
lake lilikuwa limetoa mawe. Pesa nyingine zimewekwa benki na hizi
milioni tano ni matumizi ya nyumbani na dukani.
Walibishana
wenyewe kama wabebe pesa ziwe kielelezo cha kesi ya kanda, na baada
ya kubishana wao kwa wao pesa ziliachwa nyumbani na wakaandamana na
Mama Tony kituoni.Usiku wa manane, askari wale wale walirudi
nyumbani kwa mama Tony wakidai walisahau kitu fulani ndani ya
nyumba. Walimkuta msaidizi wa nyumba, na walipofunguliwa breki ya
kwanza ikawa ni kwenye chumba cha kulala na wakapekua godoro ili
waone kama mzigo wa pesa bado uko. Walipoambiwa kwamba pesa
zimepelekwa kwa mzee Mererani usiku huo, unajua jinsi
walivyojisikia. Waliondoka shingo upande na kuwaacha wanakijiji
waliogubikwa na woga wa magari ya polisi kijijini usiku wa manane
ambapo siyo kawaida ya kijiji hicho kutembelewa na wageni kutoka
serikalini.
Asubuhi yake Mzee mwenye nyumba aliwahi mapema
polisi kuanza jitihada za kumtoa mke wake ndani hata kwa dhamana.
Mikwala aliyowekewa ilikuwa babu kubwa. Kwanza aliambiwa kwamba
shauri lao kubwa sana kwani amri ilitoka juu. Mzee wa kichagga
kutoka Mererani akaanza kutumia pesa kumtoa mke wake. Aliongea na
wazee maafande wadogo karibu wote bila mafanikio. Usisahau kwamba
maongezi yanafanyika baa na bili zote za pombe pamoja na miguu ya
mbuzi anayelipa ni Mzee wa Mererani. Wiki tatu zikakatika na mama
Tony bado yuko ndani. Baada ya kuuliza nini kinachotakiwa ndipo
alipoelekezwa amuone mkuu wa kituo. Aliyempa ushauri huo ni afande
ambaye cheo chake ni koplo jina lake tunalo. Alimwambia mkuu wa
kituo cha polisi Moshi siyo mtu rahisi kuona kwa hiyo lazima
mipango dhabiti ifanywe ili mkutano wake na mkuu wa polisi
ufanikiwe. Mzee alikubaliana na kila kitu ili mradi mke wake
atoke.
Hatimaye alifanikiwa kukutana na mkuu wa kituo cha
polisi Moshi.Mkutano ulifanyika kwenye hoteli kubwa kuliko ile
waliyokuwa wakikutana na maafande, kwa hiyo bili za vinywaji na
vyakula zilikuwa kubwa kuliko awali. Mzee wa Kichagga
alichanganyikiwa alipoambiwa kwamba shauri lake hata mkuu wa kituo
haliwezi, kwani hata yeye alipokea amri kutoka makao makuu Dar
kwamba wote watakaokamatwa na kanda za Munishi wawekwe ndani hadi
uchaguzi umalizike. Mwezi ukaisha na mama Tony bado alikuwa kituo
cha polisi Moshi. Ilimbidi mzee wa Kichagga atumie kila pesa
aliyokuwa nayo kununua uhuru wa mke wake. Hatimaye alifanikiwa
kumtoa katika kituo cha polisi, na alipokuwa akiongea nami hakumbuki
ni pesa ngapi alizotumia katika harakati za kujaribu kuununua uhuru
wa mkewe, lakini alisema ni mamilioni ya shilingi. Mama Tony
alitakiwa kuripoti polisi mara mbili kwa wiki na alifanya hivyo kwa
mwaka mzima. Mpaka wakati walipoambiwa kwamba faili ya kesi yao
imefungwa, Maisha yao hayakuwa sawa tena. Pesa zilikuwa
zimewapungukia. Biashara ilikuwa imezorota, Bado maofisa wa polisi
walikuwa wakija dukani na nyumbani kwao kila wanapoamua kufanya
hivyo.
Afya ya mama Tony ilianza kuzorota japo hakudai
kuteswa alipokuwa kituo cha polisi kwa muda mrefu. Mwenyewe alisema
hakuwahi kupigwa na askari wakati wote akiwa rumande ya polisi,
lakini anasahau kwamba haikumpasa awe hapo zaidi ya masaa ishirini
na manne bila kufikishwa mahakamani. Mwezi wa nane mwaka huu
2003 Mama Tony aliaga dunia baada ya kulalamika kwamba kichwa
kinamuuma siku moja kabla ya kifo chake. Siyo nia yangu kukihusisha
kifo chake na serikali ya CCM, lakini msomaji unaweza mwenyewe
kuangalia mchango wa CCM katika kifo cha mama Tony na ufukara wa
mume wake.
Alikuwa milionea wa Mererani, lakini baada ya
serikali kuyaingilia maisha yake sasa hana pesa. Hata nauli ya
kwenda Mererani kujaribu bahati siku hizi anaomba. Mbaya zaidi
amempoteza mke wake mwaka huu. Watoto yatima, Baba mjane, na kanda
zake hawakumrudishia. Kanda alikuwa amezinunua kutoka kwa wakala
aliyekuwa amezifuata Nairobi. Hii ndiyo CCM ambayo kila nikisema
haifai kuwa madarakani wengine hawanielewi. Nashukuru wengi
wananielewa hasa wale waliowahi kukutana ana kwa ana na mateso ya
CCM. Jamaa na marafiki wa Waislamu zaidi ya sabini waliouawa
Zanzibar wakati wa uchaguzi uliopita watanielewa nisemapo CCM ni
chama cha wauaji. Wenye maduka ya kanda walionyanganywa kanda
walizonunua kwa pesa taslimu, watanielewa kwa nini nasema CCM ni
Chama cha Majambazi.
Dawa ni kuitoa CCM madarakani kwa njia
ya kura. Kura yako ndiyo uhai wako. Usikubali kuiuza kwa pesa au
ahadi za uongo kutoka CCM. Wakikupa pesa kula lakini kura yako
usiwape CCM. Nasema pesa pokea kwani ni mali yako. CCM hawana
kilicho chao bali kila walicho nacho waliwanyanganya wananchi wa
Tanzania. Mungu amesikia kilio cha watanzania na ameanza kutusaidia
kuufikia ukombozi wetu. Mungu wabariki wananchi wa Tanzania.
Wasaidie kuitoa CCM madarakani bila umwagikaji wa damu. Watanzania
walio nje wape moyo wa kurudi kuja kuijenga nchi yetu ya Tanzania.
Tumeomba machache katika jina la Yesu. AMEN. |