Munishi
Group:
Members Posts: 78 Joined: Nov. 2003
|
"Maovu ya CCM sasa basi"
Mwinjilisti Faustin Munishi http://www.munishi.com/
CCM imeleta Jehanamu Tanzania. Watanzania watakaoingia Jehanamu,
Itabidi Mungu awapunguzie ukali wa moto kwani tayari wameungua vya
kutosha chini ya utawala dhalimu wa CCM. CCM ni wanyanganyi. Walianza
kuwanyanganya wananchi mali zao wakitumia azimio la Arusha, na sasa
Mkapa anatunyanganya mali akitumia ukusanyaji wa kodi. Anatumia
TIN kama nambari 666 ya mpinga Kristo kutunyanganya mali zetu. Je
Roho ya mpinga Kristo inafanya kazi ndani ya CCM? Kila dalili zinaonyesha
hivyo.
Wananchi wapendwa yangu ni machache sana leo. Maisha yetu na watoto
wetu ni muhimu kuliko chama chochote cha siasa. Hakuna sababu ya
kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa, wakati chama husika ndicho
sababu ya kuharibika kwa maisha yetu ya sasa na baadaye. Nazungumza
kuhusu CCM. Inasikitisha kuona kwamba wananchi Tanzania wameyazoea
maovu ya CCM kiasi cha kukata tamaa ya kujikomboa.
Kwao maovu wanayofanyiwa ni kawaida iliyozoeleka, na hawaoni sababu
ya kufanya chochote kujitoa kwenye makucha ya CCM. Niko hapa kuwapa
sababu za kuanza harakati za kujikomboa. Tunataka ukombozi kwa sababu
ni haki yetu. Lazima tujikomboe kwani tusipofanya hivyo hakuna atakayefanya
kwa ajili yetu. Maisha yetu ndiyo yanayoharibiwa, kwa hiyo hakuna
mhadhiriwa nambari moja kama mwananchi wa Tanzania. CCM inawatesa
Watanzania, wengine inawaua kosa lao ni kusema CCM itoke madarakani
kwani sera zake zimeiharibu Tanzania.
Maumivu Mateso Dhuluma Uonevu, na uchungu wote tunausikia, na mwisho
wa kuvumilia umefika. Kifo mara nyingi huwa ndio mwamuzi kati ya
uchungu na maumivu makali, huupumzisha mwili usiteseke tena. Tusipochukua
hatua kwa kuogopa kuuawa, mateso na maumivu ya CCM yatafanya kile
tunachokiogopa. Tayari yameua wengi, na wengi wako mbioni kufuatia
mkondo huo.
Swali langu kwenu ni hili: Mnataka CCM iue wangapi ndipo mseme imetosha
liwalo na liwe? Kwangu naona imetosha, SASA BASI. Liwalo na liwe,
tutachukua hatua za haraka kujikomboa. Je tuchukue hatua gani? Kwamba
tumefikia mahali pa kujiuliza swali hilo, hiyo ni hatua nzuri ya
mwanzo. Nani anayeweza kusema kwamba mateso ya CCM hayajamhadhiri
kwa lolote? Atakuwa anasema uongo. Kila Mtanzania mdogo kwa mkubwa,
ameonja maovu ya CCM.
Siyo nia yangu kuamsha hisia zenu kinyume na CCM bali nia yangu
ni kuwafanya muipende kiasi cha kuitoa madarakani. Kuitoa CCM ndani
ya mawazo yenu ni rahisi kama ilivyoingia. Swali la kujiuliza ni
Je CCM iliingizwaje kwenye mawazo na fikra zetu? Jibu lake ndiyo
njia ya kuitoa na kuisahau. Sitaki tufanye kosa la kuitoa CCM kwa
mbinu wanayoitumia kubaki madarakani. Tutakosea kwani tutakuwa tukifanya
kile wanachokijua zaidi yetu. Kwa hiyo mawazo kwamba tutaitoa CCM
kwa mtutu wa bunduki msahau.Tena hatuwezi kutumia chama kingine
cha siasa kuitoa CCM, kwani hakutakuwepo na tofauti.
TUTAITOA CCM MADARAKANI BILA SIASA
" Siasa ni uongo, kwa hiyo hatuwezi kuutumia uongo kuwatoa waongo."
Siasa ni uongo, kwa hiyo hatuwezi kuutumia uongo kuwatoa waongo.
Ndugu wananchi, asiwadanganye mtu. Hakuna siasa nzuri. Wanasiasa
wote duniani mbinu zao zinafanana tofauti ni mahali mbinu hizo zinapotumika.
Kwa hiyo rais wa Amerika hana tofauti yeyote na wanasiasa wetu hapa
Tanzania sema kiwango cha uongo wanachotumia wanasiasa wa nchi zilizoendelea
kinazidi kile kinachotumiwa na wanasiasa wa nchi zinazojaribu kuendelea.
Kifupi hakuna nchi iliyoendelea duniani.Kilichoendelea ni mbinu
za kuwaibia wananchi walio wengi mali yao ambayo ni haki yao, na
kuiingiza kwenye mkondo wa kisiasa ambao unalindwa na uongo pamoja
na silaha kali. Kwa hiyo mbinu ya kwanza kuwatoa CCM madarakani
ni kutambua kwamba wanasiasa wote duniani ni waongo. Pili ni kutokusikiliza
uongo wao ambao hupeperushwa na vyombo vya habari kila siku. Ni
vizuri mjue kwamba hakuna vyombo huru vya habari katika dunia inayoongozwa
na siasa. Kwa hiyo someni habari magazetini, pia sikilizeni redio.
Lakini mjue asilimia tisini ya yale mnayoona na kusikia kwenye vyombo
vya habari ni takataka kama siyo uongo na mbinu za kuwafanya mnunue
bidhaa. Kwa sababu wanasiasa wengi siyo waandishi wa habari, kazi
hiyo hufanywa na wanataaluma hiyo kwa malipo.
Kwa hiyo hamtakosea kama mtasema kwamba waandishi wa habari wameshirikiana
na wanasiasa kuifikisha hali yetu kimaisha ilipo. Uzuri wa waandishi
wa habari, ni kwamba wanaweza kirahisi kurudiwa na fahamu zao, na
kuwageuka wanasiasa na kuungana na sauti ya wanainchi. Tatizo ni
kwamba walikuwa hawajui kama mnajua. Wakijua kwamba nimewaambia
na mbaya zaidi wajue kwamba sasa mnajua yale waliyowaficha muda
mrefu, watajikomba kuwaumbua wanasiasa. Hapo tuwe tayari kusikia
mengi. Watakapogeukana hiyo ni furaha tele upande wetu.Tutakuwa
tumempata msaidizi katika vita yetu ya kuwatoa CCM madarakani.
WANASIASA HUTUMIA VYOMBO VYA DOLA KUWANYANYASA WANANCHI "Kila inapobidi
majeshi yote hutumika kulinda maslahi ya wanasiasa. "
Siyo rahisi wanasiasa warudiwe na fahamu zao, hasa ukitilia maanani
kwamba wamezoea ukubwa na kutaka kuabudiwa kama 'miungu' wadogo.
Kwa hiyo watatumia kila mbinu kubaki madarakani. Mbinu wanayoijua
zaidi ni ile ya kutumia vyombo vya dola kama polisi na majeshi yote
ya angani nchi kavu na majini, bila kusahau vikosi vya siri ambavyo
hutumiwa kuwanyamazisha wapinzani.
KAZI IKO HAPA.
Wananchi wapendwa sipendi kuwaficha niwaambie kibarua kilicho mbele
yetu ni rahisi. Nitakosea sana nikifanya hivyo. Jukumu langu ni
kuweka wazi mbele yenu kila pingamizi tutakalokutana nalo, na kuwaeleza
mbinu na njia sahihi ya kupambana na adui yetu. Majeshi yote yameundwa
na wananchi wa TANZANIA. Polisi kwa lengo la kulinda mali zetu wananchi,
na majeshi yale mengine wanasema lengo lao ni kulinda mipaka ya
nchi yetu.
Hiyo ndiyo lugha wanayotumia wanasiasa kutuonyesha kwamba majeshi
yako kwa ajili yetu wananchi kumbe ni kinyume chake. Kila inapobidi
majeshi yote hutumika kulinda maslahi ya wanasiasa. Mnakumbuka yaliyowapata
wananchi wa Zanzibar walipojaribu kuipinga CCM. Wananchi zaidi ya
sabini walipoteza maisha yao, huku wengine wakikatwa viungo vya
miili yao ili kuwafundisha adabu.
Yaani watanzania wako tayari kuua wenzao kwa ajili ya wanasiasa.
Hiyo ndio kazi iliyo mbele yetu. Mjue kuna watu walio tayari kuua
kwa ajili ya CCM na viongozi wake. Na tayari walifanya hivyo mchana
jua linawaka bila kuogopa kamera za TV. Inataka moyo, lakini msisahau
nguvu iliyo katika KWELI. Ukweli utatuweka huru mbali na wanasiasa
waongo. Kweli ni NENO la Mungu ambalo ndiyo silaha yetu yenye nguvu
zote.
TIINI MAMLAKA HATA CCM?
"Tuna haki na uhuru wa kuikataa CCM, na Mungu aliyetupa hawezi kutunyanganya
haki na uhuru huo. Ni mali yetu, aliyetupatia ni Mungu na tumeamua
kutumia haki na uhuru huo kuikataa CCM ya wauaji. "
Wacheni waje wakitumia silaha, sisi tutawakabili kwa NENO la Mungu.
Kwa imani yote yawezekana kwa waaaminio. Imani yetu kwa Mungu tusikubali
iyumbishwe na chochote. Siyo matisho ya CCM wala kejeli zao.Mara
zote wananchi ndio wengi kuliko risasi zote CCM walizojilimbikizia.
Sauti ya wengi ndiyo sauti ya Mungu.
Tukisema kwa sauti kubwa kwamba 'CCM CHAMA CHA MAJAMBAZI HATUKITAKI,'
hiyo ndiyo itakayokuwa sauti ya Mungu. Na hakuna awezaye kushindana
na MUNGU. Tuna haki na uhuru wa kuikataa CCM, na Mungu hawezi kutunyanganya
haki na uhuru huo. Ni mali yetu, aliyetupatia ni Mungu na tumeamua
kutumia haki na uhuru huo kuikataa CCM ya wauaji. Watakaopingana
na uamuzi wetu kuikataa CCM, hao ndio watakaokuwa wakipingana na
agizo la Mungu. Ndiyo watakuwa wameasi mamlaka ya Mungu. Kwa hiyo
lazima waitii mamlaka yetu wananchi, kwani hiyo ameiweka Mungu mwenyewe.
CCM iliwekwa na mtu mmoja, ni sawa ikitolewa na watu.
Walitudanganya kwamba wanafanya uchaguzi ili iwe kana kwamba iliwekwa
na watu, lakini tumegundua janja yao.Maoni ya wengi hayajawahi kuheshimiwa
katika uchaguzi wowote ule tuliowahi kuwa nao. Kwanza tulikuwa tukichagua
nini kinyume cha nini? Uchaguzi lazima uwe kati ya Shetani na Mungu,
na siyo kati ya shetani na mashetani. Chaguzi tulizowahi kuzifanya
kabla ya vyama vingi vya siasa, zilikuwa kati ya Shetani na kivuli.
Chaguzi tulizofanya wakati wa vyama vingi vya kisiasa, zimekuwa
kati ya Shetani {CCM}na vijishetani {vyama vya upinzani} ambavyo
navyo vitakua kumfikia Shetani mwenyewe. Sasa tunataka uchaguzi
wa kweli. Tuchagua kati ya Shetani na Mungu. Duniani hakuna uchaguzi
zaidi ya kuchagua MUNGU na Shetani. Hakuna kitu cha tatu wananchi
msidanganyike.
GIZA NA NURU
" Msije mkanilaumu kwamba nilisema siasa ni dini ya shetani."
Dunia imekuwa na historia ya kupenda giza kuliko NURU, ndio maana
wengi wanapenda siasa ambayo ni giza nene. Nuru ya injili sasa inaangaza
duniani kote. Inatufundisha kuikataa siasa ambayo hutumiwa na shetani
kuyatekeleza malengo yake ya kuharibu, kuchinja na kuua. Msije mkanilaumu
kwamba nilisema siasa ni dini ya shetani. Lakini hata kama ulimi
wangu ungeteleza niseme hivyo, ningekuwa nimekosea nini? Je sasa
nimesema hivyo? Hapana. Nilichosema ni kwamba siasa ni chombo anachotumia
sana Shetani. Hatuwezi kumkataa Shetani na kuikubali SIASA chombo
anachokitumia. Tumkatae jongoo na mti wake. Wananchi! Siasa ni mbaya
na hilo mnalijua fika. Wengi mtaniuliza nini mbadala wa siasa? Jibu
langu ni KWELI. Neno la Mungu ndiyo KWELI.
UJAMAA NA UBEPARI
"Ujamaa ulisikika mzuri masikioni, lakini kwa sababu aliouleta alikuwa
Nyerere mwanasiasa muongo, kila kilichovutia hakikutekelezeka."
Watu tofauti kwa nyakati tofauti wamekuwa na mawazo tofauti kuhusu
mfumo gani unaofaa kumwongoza mwanadamu. Wengine waliufuata mfumo
wa ukomunisti kama akina Nyerere, wakashindwa kabisa. Mbaya zaidi
walitumia miaka zaidi ya 30 kuyajaribu mawazo yao ya ujamaa Tanzania.
Matokeo yake yalikuwa kuiacha Tanzania ikiwa imeharibiwa na sera
zao mbovu, na hata sasa hatuna sera kamili tunayoifuata.
Tanzania siyo mabepari wala siyo wajamaa kama alivyotaka Nyerere.
Sisemi ubepari ni bora kuliko ujamaa, kwani sera zote hizo ni za
kisiasa. Kwangu zote ni mbovu kwani zinakosa KWELI ndani yake. Ujamaa
ulisikika mzuri masikioni, lakini kwa sababu aliouleta alikuwa Nyerere
mwanasiasa muongo, kila kilichovutia hakikutekelezeka. Badala ya
aliyeanzisha kukiri kwamba alikuwa amesema uongo, alitumia uongo
mkumbwa kuutetea uongo mdogo aliouanzisha. Miaka ikapita na tulichoambulia
watanzania ni umaskini wa kutisha.
Nyerere alitutaka tuamini kwamba dunia yote inapita kwenye matatizo
kama yetu watanzania, na wakati huo huo polisi waliwakamata wananchi
waliopatikana na sabuni, dawa za meno na mafuta ya kupikia kutoka
Kenya. Ilikuwa ni sawa na kukamatwa na madawa ya kulevya. Wengi
wakati huo tuilijiuliza: Ikiwa dunia yote ina mateso kama yetu,
mbona hapa Kenya wao wanaogea sabuni? Tofauti na sisi tunaotumia
maziwa ya mpapai kuogea? Tena mbona wenzetu wanatumia dawa za meno
wakati Nyerere anaziita anasa? Kweli kuogea sabuni ya REXONA au
kutumia dawa ya meno ya COLGET ni anasa? Nyerere mwanasiasa muongo
alitutaka tuamini hivyo.
Wengi walimuamini na mpaka leo hawataki makuu. Waliukubali umaskini,
na hawataki kuchukua hatua zozote kupambana nao. Japo Nyerere alisema
adui zetu ni umaskini ujinga na maradhi, alitufundisha kuwapenda
na kuwakubali maadui hao. Nasikitika kusema kwamba kuna watu waliomwamini
Nyerere kinyume cha Amin wa Uganda. Waliomwamini Nyerere walikosea
sawa na waliomwamini Amin. Watu hao wawili walileta madhara kwa
nchi zao, lakini ya Nyerere Tanzania yalizidi.
Ninachotaka kusema ni kwamba mifumo yote ya siasa ilishindwa. Sasa
tuufuate mfumo wa Injili ambao hauwezi kushindwa. Injili ni uwezo
wa Mungu, sioni haya kusema Injili ndio mkombozi wa dunia. Itaikomboa
dunia kutoka katika minyororo ya uongo ya wanasiasa. Lazima tuiamini
Injili kama kweli tunataka ukombozi. Dunia ni ya Mungu na haiwezi
kuongozwa kwa siasa za watu ambazo ni uongo. Dunia itaongozwa na
KWELI ya neno la MUNGU.
WANASIASA NA MFUMO WA BIASHARA NCHINI
"Inasikitisha kuona wananchi ndani ya nchi yao wakiteseka, huku
wanasiasa na wageni wachache wakimiliki njia zote kuu za uchumi."
Duniani kuna vita nyingi na tetesi za vita. Yote hayo ni matunda
ya wanasiasa. Shetani anawatumia kuua na kuharibu maisha ya watu.
KWELI imekuja ili tuwe na uzima, kinyume na shetani aliyekuja kuua.
Utajiri wa dunia uko mikononi mwa wanasiasa. Mnajua ni kwa nini?
Ili utajiri huo utumike kununua kila wanachokihitaji. Nanyi wananchi
ni moja ya bidhaa ambayo wanasiasa hupanga kuinunua. Mnanunuliwa
wakati wa kura ili kutia saini chaguzi ambazo washindi hujulikana
kabla ya siku ya kura.
Hawataki mjiendeleze ili muwe rahisi kununuliwa. Ndio maana wengi
wenu hamjiwezi kimaisha na hiyo haiwasumbui wanasiasa kwani wanapenda
mbaki kama mlivyo ili wawatumie. Hata wale wanaojaribu kujipatia
riziki zao za kila siku kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo, bado
wanasiasa hawaachi wafanye hivyo. Kila siku tume ya jiji hupewa
kazi ya kuusafisha mji, na wafanyabiashara ndogo ndogo ndio uchafu
unaotakiwa kusafishwa mijini. Siyo ajabu kwani huo ni mpango kamili
unaolenga kuwanufaisha wafanyibiashara waliounganishwa kisiasa.
Hawa ndio wale ambao hupewa tenda za serikali ili wagawane mapato
na wanasiasa.
Kuna wengine wa asili ya kiasia ambao nao hupewa kumiliki maeneo
yote muhimu ya kibiashara. Makubaliano ni kwamba mapato wayagawane
na wanasiasa. Inasikitisha kuona wananchi ndani ya nchi yao wakiteseka,
huku wanasiasa na wageni wachache wakimiliki njia zote kuu za uchumi.
Hali hii haipaswi kuwa hivyo. Wananchi wanatakiwa wapewe uhuru wa
kufanya biashara popote katika nchi yao. Udogo wa biashara usiwe
ndio sababu ya kumsumbua mwananchi, kwani hata hizo biashara kubwa
ziliaza zikiwa ndogo. Wananchi wanaoiamini KWELI wanatakiwa waruhusiwe
kufanya chochote chema katika nchi yao.
Hali hiyo ndio itakayochochea ubunifu utakaopelekea kugunduliwa
kwa vitu vingi kwa ajili ya maisha ya kila siku ya mwanadamu. Ugunduzi
huo ndio unaoweza kuinua uchumi wa nchi husika kinyume na nchi nyingine,
kwani "akili ni nywele na kila mtu ana zake." Na wale wanaogundua
vitu, wanapaswa kulipwa sawa sawa na ugunduzi wao. Hapo taifa litakuwa
limejitengenezea wanasayansi wake, wanaoweza kuvumbua vitu ambayo
wengine hawana, na wakiviitaji taifa linapata pesa za kigeni kuinua
uchumi wa nchi.
Sekta ya elimu nayo itakuwa imeboreshwa kwani elimu kwa watoto wetu
itazingatia zaidi vitu tulivyogundua wenyewe, kinyume na elimu ya
sasa ambayo misingi yake ni mengi yaliyofanywa na wengine, huku
tukipima uwezo wetu katika kuyaiga. Ndiyo maana maisha ya waalimu
katika nchi nyingi ni duni. Wanasiasa hufundishwa na waalimu, lakini
kimaisha wametofautiana sana. Waalimu mishahara yao ni midogo sana
kulinganisha na wanasiasa ambao kila kukicha hujiongezea mishahara
na marupurupu mengi.
Katika nchi ambayo inaongozwa na KWELI bila siasa, waalimu ndio
wanaotakiwa kupata mshahara wa kuwatosha kumudu maisha yao kama
siyo uliowazidi wanasiasa. Hata kama watawazidi wanasiasa kimshahara
kuna ubaya gani? Hilo ni swali tu. Msije mkasema niliwaambia mishahara
ya waalimu izidi ya kila mtu. Lakini waalimu ndio humfundisha kila
mtu. Sasa inakuwaje kila mtu anampita mwalimu kimshahara? Hapo nimetoka
maana naona maswali hayaishi kichwani mwangu. Mengine mtajijazia
wenyewe.
RAIS BILA WALINZI?
Watalinda nini wakati KWELI inajilinda yenyewe?
KWELI na uongo ni kama mafuta na maji. Huwezi kuvichanganya hata
kama utajaribu kufanya hivyo. Kweli inajilinda yenyewe na haihitaji
kulindwa na silaha kali. Uongo lazima ulindwe kwa kutumia silaha
kali, kwani hawajui wale waliodanganywa wakierevuka watafanya nini.
Ndio maana dunia nzima inafikiria kuhusu silaha kali kuliko chakula
cha wanadamu wanaoikaa. Waangalie wanasiasa wanavyolindwa. Watu
zaidi ya mia moja hawafanyi kitu kingine duniani ila kumlinda mwanasiasa.
Naheshimu kila taaluma ya mtu, lakini siwezi kumshauri yeyote awe
mlinzi wa mwanasiasa. Kwa nini ufe kwa ajili ya uongo ambao hukuusema?
Tena kwa mshahara gani basi? Yaani wenzio wako ndani wanakula vinono
nawe unaungua jua nje? Sawa ni kazi yako. Unaipenda. Sina la kuongeza.
Lakini ikiwa mimi ndiye nitakayekuwa kiongozi katika nchi itakayokuwa
ikiongozwa na KWELI bila siasa, basi sitaki walinzi. Watalinda nini
wakati KWELI inajilinda yenyewe?
Unamkumbuka mmoja wa wanafunzi wa Yesu aliyejaribu kufanya kazi
ya kumlinda? Alikata sikio la mmoja wa askari waliokuwa wanamkamata
Yesu. Aliambiwa aurudishe upanga wake kiunoni kwani YESU ni KWELI
iliyotoka kwa Mungu na hakuhitaji kulindwa na mapanga au bunduki.
Pesa wanazotumia wanasiasa kununulia silaha za kujilinda, zinatosha
kumaliza baa la njaa duniani kote.
Yaani nina maana kila mtu duniani anaweza kula milo mitatu kwa siku.
Tena chakula kizuri. Lakini pesa zote wanatumia wanasiasa kununulia
silaha kali za kujilinda na wale waliowadanganya. Mwisho wao umefika.
KWELI itawatoa madarakani bila kutumia silaha. Ole wao. Silaha walizojiwekea
watazifanyia nini? Mbinu za vita zimebadilika. Hatutatumia mbinu
walizozizoea.
Nguvu ya kweli ya INJILI itawakata makali yao. Injili ni NENO la
Mungu ambaye ndiye KWELI yenyewe. Je wanasiasa watashindana, au
kupigana na Mungu? Kila la kheri katika vita yao hiyo. Watatoweka
mmoja baada ya mwengine. Hawatajua ilikuwaje, wala hawaruhusiwi
kujua. Pesa na utajiri havitawasaidia wakati huo. KWELI haipimi
uzito wa mtu kulingana na vitu alivyo navyo. Mtu ni mtu hata kama
hana vitu. Mtu huunda vitu, lakini vitu haviwezi kuunda mtu. Vitu
ni kwa ajili ya mtu, lakini siyo mtu kwa ajili ya vitu.
WANASIASA HUTUMIA DINI KUTAWALA
Makanisa mengi yameanzishwa na kufadhiliwa na wanasiasa kwa kwa
lengo la kuyatumia kisiasa, wakati lugha yao ni kwamba chama na
serikali havina dini.
Dini ni imani kwa Mungu wakati siasa ni imani kwa watu. Zote mbili
ni itikadi zinazohitaji watu kufanikisha malengo yao. Ndio maana
nawataka watu wa dini zote tuungane pamoja kuitoa siasa madarakani.
Suala kwamba dini gani itatawala hilo lisitusumbue kwa sasa. Muhimu
ni wote tutambue kwamba wanasiasa wanatutumia vibaya. Baada ya kutambua
hayo tuachane kabisa na siasa. Kitakachofuata ni kila dini inayowania
uongozi kujitokeza hadharani na kutangaza nia yao ya kutaka kuongoza.
Wananchi wa dini husika, pamoja na wale wasio na dini, bila kuwasahau
wale wa dini nyingine watakaoamua kujiunga na dini yenye sera nzuri
kutoka kwa Mungu, Watachagua dini gani iongoze kwa kipindi kilichozoeleka
cha miaka mitano.
Baada ya miaka mitano tutachaguana tena. Pamoja na kwamba kila dini
itakuwa na katiba yake, lakini lazima tuwe na katiba moja ya pamoja.
Nayo ni ile itakayozingatia Imani kwa Mungu ambayo ndilo lengo la
kila dini. Pamoja na kwamba dini fulani itachukua uongozi kwa kipindi
cha miaka mitano, bado kila dini itawakilishwa katika baraza la
makuhani ambalo ndilo litakalohusika na kuhakikisha kwamba amri
kumi za Mungu zinafuatwa kikamilifu. Kwa hiyo hofu kwamba kutatokea
michafuko ya kidini msahau kabisa. Badala yake dini zote zitaingia
katika ushirikiano ambao haujawahi kuonekana tangu kuumbwa ulimwengu.
Bado kila dini itakuwa huru kuendelea kufanya mambo yake yenyewe,
bila kuomba kibali kwa wanasiasa kama ilivyo sasa.
Hakutakuwepo na makanisa ua misikiti inayodhaminiwa na serikali.
Makanisa mengi yameanzishwa na kufadhiliwa na wanasiasa kwa kwa
lengo la kuyatumia kisiasa wakati lugha yao ni kwamba chama na serikali
havina dini. Mambo yako hivyo karibu kila dini. Inasikitisha kuona
kwamba wengine wanafikia mahali pa kudanganya kwamba watu wamepona
kwenye mikutano yao ya kidini, kumbe ni waongo. Tayari tumewangundua
kuwa ni wapambe wa CCM. Wanalindwa kama wanasiasa na huku wanajiita
maaskofu. Wanatembelea magari ya kifahari na huku waumini wao ni
masikini wanaodanganywa kwamba wakitoa watabarikiwa. Tayari viongozi
wa dini wanawasaidia wanasiasa katika kuendeleza ukandamizaji na
uonevu kwa waumini wao, ili mradi tu waitwe ikulu na wapewe magari
na pesa. Hawana tofauti na wanasiasa tunaotaka kuwatoa madarakani.
Kweli ya Mungu ni taa. Ikiwamulika, matendo yao yataonekana na kila
mtu. Hawa ndio watakaokwenda pamoja na wanasiasa wakati dini ya
kweli itakapochukua madaraka.
MAUAJI YA KISIASA SIRI YAFICHULIWA
Wanasiasa kwa makusudi wameziharibu taasisi zote. Duniani taasisi
zote hufanya kazi kwa ajili ya wanasiasa. Nchi zilizoendelea wameendelea
katika kujaribu kuficho hilo lakini nchi zetu jambo hilo liko wazi.
Kwamba wana mbinu kali za kulificha, haiwatofautishi na wenzao katika
nchi zinazoendelea. Inabaki kwamba kila taasisi duniani inalinda
maslahi ya wanasiasa kwanza. Mahakama mara nyingi zinaonekana kupindisha
ukweli, hasa pale ambapo mwanasiasa anahusika. Hebu fikiri kuhusu
gari lililotekwa nyara katikati ya mji.
Watekaji wanamlazimisha mwenye gari kuliendesha kuelekea wanakotaka.
Baada ya safari ya kama kilomita mbili hivi, wanaacha gari la kwanza
baada ya kulizinga jingine kwa mbele. Mwanye gari la pili anapigwa
risasi na kuuawa hapo hapo baada ya kisichojulikana kuendelea kati
ya watekaji na yeye. Wanayaacha magari yote mawili hapo baada ya
kumwamuru mwenye gari la tatu kutoka ndani ya gari lake na kuwapa
funguo. Wanaondoka na gari huku wakiwaacha wenye magari wote mahali
pamoja, lakini mmoja ni marehemu na mwingine amebaki bila gari.
Baada ya dakika kama tano hivi, Polisi wanawasili mahali hapo. Wakiwa
katika kuwahoji wenye magari wawili, waandishi wa habari wa magazeti
TV na Redio wanawasili mahali pa tukio. Usijali wataulizana nini
hapo, lakini sikiliza redio na utizame TV jioni, halafu usome magazeti
asubuhi yake. Utakayemsikia akitajwa kwamba aliuawa na majambazi
waliojaribu kumpora gari, ndiye aliyekuwa amelengwa na taaluma zote
hizo. Yaani habari yenyewe itasomeka hivi. MAJAMBAZI WAMUUA BWANA
XXXX Aliyekuwa mhubiri wa INJILI bwana XXXX amefariki dunia baada
ya majambazi kumfyatulia risasi.
Wakiongea katika sehemu ya tukio, bwana JJJJ na bwana SSSS walisema
kwamba walishuhudia majambazi wakimfyatulia risasi bwana XXXX baada
ya mvutano ulioonekana kama Bwana XXXX alikataa kuwapatia majamabzi
fungua za gari lake. Wakisimulia saidi kisa hicho, walisema kwamba
walisikia mlio wa risasi mara mbili, na baadaye majambazi walitoka
kwenye gari la huyo aliyekuja kujulikana baadaye kama Bwana XXXX.
Walimwamuru Bwana SSSS atoke kwenye gari lake na awape funguo. Alitii,
na majambazi waliondoka na gari lake ambalo mpaka sasa halijapatikana.
Kwa sababu vyombo vyote vya habari vimelipa uzito suala hilo kwenye
kurasa zao za kwanza, wananchi wanaiamini hadithi hiyo. Ndiyo lengo
lilikuwa ifanyike hivyo ili wananchi waaminishwe uongo. UKWELI wa
mambo ni kwamba bwana XXXX alikuwa mlengwa kwenye sakata yote hiyo.
Kuna mtu aliyejua kwamba atapitia barabara hiyo saa hizo baada ya
kutafiti nyendo zake kwa zaidi ya miezi mitatu. Taasisi zilizotumika
kuwadanganya wananchi nazo zilihusishwa wengine wakijua na wengine
bila kujua. Walioporwa magari yao ndio ambao hawakujua nini kilichokuwa
kikiendelea. Ilikuwa hivi: Bwana XXXX aliwaudhi wanasiasa kwa kujaribu
kuwaambia kwamba wanasiasa hawawatendei mema wananchi walio wengi.
Walipochukizwa naye wakaamua kwamba atauawa. Pesa nyingi zikatolewa
kwa ajili ya kazi hiyo. Walitakiwa watu kutoka katika taasisi mbili
nyeti. Polisi na vyombo vya habari vilitosha kukamilisha zoezi zima.
Kachero mmoja wa polisi alitumika kuzijua nyendo zote za Bwana XXXX,
halafu mkuu moja wa kituo cha polisi alitakiwa kuwatoa vijana ambao
watafanya kama wafanyavyo majambazi. Na huyo huyo ndiye aliyetakiwa
kuvipigia simu vyombo vya habari kuviarifu kuhusu tukio, na jitihada
zao za kuwafukuza majambazi.
Lengo likiwa kutekeleza mauaji ya kisiasa, na kuyafanya yaonekane
kama ujambazi wa kawaida. Walikosea. Kwanza hakuna ujambazi wa kawaida.
Kwamba kuna ujambazi hiyo inaonyesha kushindwa kwa wanasiasa kuwalinda
wananchi pamoja na mali zao. Pili: Kwamba wanamuua mtu kwa sababu
tu amewakosoa chama tawala CCM huo ni wendawazimu nambari ONE. Wananchi
mfano huu unaonyesha jinsi wanasiasa wanavyoweza kuzitumia taasisi
kuyaficha maovu yao. Hii ni siri iliyofichuliwa katika mijadala
ya Internet huko BCSTIMES .COM baada ya siri hii kufichuliwa na
mtu aliyejiita AISHA AIESHI. Unaweza kujisomea mwenyewe kisa hicho
kwa KUBONYEZA HAPA. Kuna matukio mengi ya zamani na hivi karibuni
yanayofanana kabisa na mfano huu. Mauaji ya watu zaidi ya sabini
kule Zanzibar, Kifo cha SOKOINE aliyekuwa waziri mkuu wakati wa
Nyerere. Kifo cha KOMBE aliyekuwa mkuu wa kikosi cha usalama wa
taifa wakati wa Nyerere, na wengine wengi.
Mchungaji Faustin Munishi ambaye pia ni mwimbaji maarufu wa nyimbo
za injili Afrika ya mashariki na kati, ametangaza azma yake kuwania
kiti cha urais Tanzania katika uchaguzi ujao. Mengi yamesemwa kuhusu
hatua ya mchungaji huyo, na hapa ni sehemu ya mjadala katika mtandao.
Inasemekana serikali ilikuwa imeufungia mjadala huu usiweze kusomwa
na Watanzania. Gazeti la Injili kwenye internet linakuletea mjadala
huo bila kuhariri chochote.
SASA BASI INATOSHA
Ndugu wananchi yangu yalikuwa hayo machache. Msimame imara, wala
msikubali kuyumbishwa na hawa wanasiasa. Mkatae kabisa mbinu zao
za kutaka kuendeleza maovu yao kwa kuachiana viti. Nyerere alituachia
MKAPA ili alinde madhambi yake.Naye Mkapa anataka kutuachia sijui
nani ili alinde madhambi yake. Watalindana mpaka lini? Mwisho wao
umefika.Sasa tunataka dunia isiyo na kitu kinachoitwa SIASA.
Wametudanganya vya kutosha, wakatuibia vya kutosha sasa tunataka
KWELI ya neno la Mungu iongoze Tanzania. Mungu ni pendo na anaipenda
Tanzania ndio maana amenituma mtumishi wake kuwaletea ujumbe huu.
Msijali kufurukuta kwao kwani wangefanyaje nao wanakata roho? Watawapeleka
kwenye madanguro yao kuwatesa lakini msikate tamaa. Watatumia kila
mbinu ikiwepo ya kuwafungulia kesi za uongo, msijali kwani hayo
yote hayana budi kuja. Nguvu ya dola ni ndogo sana ukilinganisha
na nguvu ya wananchi wamoja.Umoja wetu na imani yetu kwa Mungu ndiyo
silaha kubwa ambayo kila mmoja wetu lazima awe nayo.
Watahangaika kujua nani anayetupa nguvu tulizo nazo, lakini jibu
watakalolipata litawarudisha hatua mia tatu nyuma. Wataanzisha magazeti
kwa lengo la kuueneza uongo wao lakini watagonga mawe kwani wananchi
tumeyashitukia magazeti ya hivyo. Watatumia pesa walizoiba kwetu
kutununua kwazo, nasi tutatumia pesa bila kuwaunga mkono.Pesa ni
zetu. Zikirudishwa hatuachi. Tutazitumia. Tuanze mara moja zoezi
la kuchoma moto kadi za vyama vya kisiasa. Sisi ni waumini wa dini
na hiyo inatutosha. Hatuwezi kuamini katika dini mbili, yaani siasa
na INJILI. Moja ni ya shetani na nyingine ni ya Mungu.Sisi tumeamua
kuwa upande wa Mungu. Mungu hawezi kutuacha watoto wake tuteswe
na siasa za yule mwovu.
Hatua ya kwanza tutakayoichukua kuelekea ukombozi, Mungu atachukua
hatua mia moja kutulinda na CCM pamoja na wanasiasa waovu. Mara
zote Mungu hafanyi chochote kutulazimishia matakwa yake. Lakini
tunapoamua kwamba tutaifuata njia hii, na kisha tuombe baraka na
ulinzi kutoka kwake, mara moja Mungu hutujibu maombi yetu kwa kuanza
kutulinda na kutupa ufunuo zaidi. Nilipochukua kalamu kuanza kuandika
haya, ndipo ufunuo wote huu uliponijia kutoka kwa Mungu. Ningengoja
ufunuo kwanza ndipo niandike, pengine mpaka mwaka 2080 ndipo ningepata
ufunuo huu. Ni muhimu sana kutilia maanani ujumbe huu. Huwezi kuusoma
popote kwani lengo kubwa la serikali ni kuwazuia wananchi kujua.
Wanajua kwamba mkijua mtawauliza maswali wasiyopenda kuulizwa. Wana
mengi ya kuficha na anayejaribu kuyafichua ni adui wao nambari moja.
Kama hawatammaliza kibiashara au kisiasa, basi watapanga njama za
kuutoa uhai wake. Wameuawa wengi ndiyo maana hatuchukulii kama mzaha
matisho yao ya kuua. Bonyeza hapa usome yale waliyokusudia kumfanyia
mwandishi wa hotuba hii.[/B][B]
Mchungaji Faustin Munishi.
|